Home JUHUDI ZA RAIS SAMIA ZAIPELEKA MBELE SEKTA YA MADINI

JUHUDI ZA RAIS SAMIA ZAIPELEKA MBELE SEKTA YA MADINI

GEITA.

Imeelezwa kuwa, maendeleo katika ya Sekta ya Madini yanatokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika shughuli madini.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Jamuhuri William wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 5 ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita.

Wiliam amesema juhudi hizo ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi na usimamizi mzuri wa Sera na Sheria ya Madini.

Aidha, William amesema ni muhimu kuzingatia matumizi ya zana za kujikinga wakati wa uchimbaji na uchenjuaji kwa lengo la kulinda afya na usalama wa wachimbaji, wachenjuaji na Jamii inayozunguka eneo linalofanyika shughuli za madini.

“Naomba nitumie fursa hii kuwataka wachimbaji wadogo wa madini kushiriki kikamilifu katika maonesho haya ili kupata elimu na ujuzi wa namna bora ya kujilinda wakati wa uchimbaji ili mwisho wa siku warudi nyumbani wakiwa salama,” amesema William.

Pia, William ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kujifunza na kupata huduma mbalimbali zinazotolewa katika maonesho hayo ikiwemo elimu ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Kwa upande wake, Mhandisi Uchenjuaji Madini wa Wizara ya Madini Abedi Kidindi amesema Sheria ya Madini iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2017 imeweka usimamizi na matumizi wa vilipuzi kuwa chini ya Wizara ya Madini ambapo Wizara hiyo inatoa vibali kwa ajili ya matumizi ya vilipuzi.

Maonesho ya Kimataifa ya 5ya Teknolojia ya Madini 2022 mkoani yalianza tarehe 27 Septemba 2022 na yanatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 03 Oktoba 2022.