Home LOCAL MPANGO WA ELIMU YA AFYA SHULENI UTASAIDIA KUWAKINGA WANAFUNZI DHIDI YA MAGONJWA...

MPANGO WA ELIMU YA AFYA SHULENI UTASAIDIA KUWAKINGA WANAFUNZI DHIDI YA MAGONJWA – DKT. KWESI



Na: WAF – DOM

KAIMU Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Elius Kwesi amebainisha kuwa, Mpango wa Taifa wa elimu ya Afya Shuleni utasaidia kwa kiasi kikubwa katika mapambano dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya yakuambukiza kama UKIMWI.

Dkt. Kwesi amebainisha hayo leo Aprili 28, 2022 wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri wa kitaalamu ya mpango wa Taifa wa Elimu ya Afya Shuleni kilichofanyika Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Wataalamu kutoka Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI, Wizara ya Elimu na Wadau mbalimbali.

Amesema, shule ni kati ya taasisi muhimu za mwanzo katika kutengeneza tabia ya mtoto, hivyo kuwa na mpango huu wa Elimu ya Afya Shuleni itakuwa ni msaada mkubwa katika kujenga jamii salama yenye uwezo wa kupambana dhidi ya magonjwa.

“Taasisi ya Shule ndio msingi wa kujenga tabia kwa wanafunzi, ndio maana Serikali ikaona umuhimu wa kuwa na mpango huu wa afya Shuleni utaokuwa msaada katika mapambano dhidi ya magonjwa katika ngazi ya shule na jamii kwa ujumla.” Amesema Dkt. Kwesi.

Mbali na hayo Dkt. Kwesi amesema, Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza shughuli za elimu ya afya kwa umma ili kuelimisha na kuhamasisha jamii ikiwemo wanafunzi kupambana na kujikinga dhidi ya magonjwa yanayoambukiza, yasiyoambukiza, masuala ya lishe, huduma za uzazi na mtoto na afya mazingira.

Aidha,  amesema, Wizara inatambua kuwa huduma bora za afya shuleni ni moja ya uwekezaji kwa jamii yenye umri mdogo kwa lengo la kuwa na raia wenye afya na uwezo wa kujenga Taifa kwa kuwawezesha kujifunza na kufanya vyema katika masomo yao.

Pamoja na mafanikio ya Serikali na Wadau katika kuimarisha afya na ustawi wa vijana Shuleni bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji nguvu ya pamoja kuzitatua kama vile ongezeko la maambukizi ya VVU kwa vijana kati ya umri wa miaka 10-19 , mimba za utotoni  unyanyasaji wa kijinsia, upungufu wa damu pamoja na magonjwa yasiyoambukiza. Amesisitiza Dkt. Kwesi.

Nae Kaimu Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya Dkt. Amalberga Kasangara amesema, mapambano dhidi ya magonjwa katika shule yanahitaji ushirikiano wa karibu wa Sekta zote za Serikali pamoja na Wadau ili kuweza kufikia lengo la kuwalinda wanafunzi na jamii dhidi ya magonjwa.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la UNESCO nchini anaeshughulika na masuala ya UKIMWI na Elimu ya afya Bw. Mathias Herman amesema Shirika hilo litaendelea kufanya kazi na Serikali katika eneo la kutoa Elimu ya afya ili kuwakinga wanafunzi na jamii, na kubainisha kuwa Shirika hilo litaendelea kuwezesha vikao vya kitaalamu vitavyoleta tija katika kuwalinda wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Mwisho.

Previous articleWAZIRI UMMY AMUAGA MWAKILISHI MKAZI WA WHO ALIYEMALIZA MUDA WAKE NCHINI.
Next articleELIMU MTANDAO ITUMIKE KUBORESHA USIMAMIZI WA MNYORORO WA BIDHAA ZA DAWA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here