WAZAZI na walezi mkoani Ruvuma,wametakiwa kuwapa misingi Bora watoto wao waliopo shuleni kwa kuwaunganisha na mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) ili waweze kuwa na uhakika wa kupata matibabu pindi wanapougua.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF)mkoani Ruvuma Hance John, wakati akizungumza katika kikao maalum cha wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule ya Sekondari ya Wasichana Mbinga(Mbinga Girls) wilayani Mbinga.
Hance alisema, zawadi bora kwa watoto ni pamoja na kuwaunganisha katika mfuko huo kwani utamwezesha kuwa na uhakika wa matibabu akiwa shuleni, badala ya usumbufu wa kurudi nyumbani ili wazazi wampeleka Hospitali, au kuwabebesha mzigo walimu kutumia fedha zao kwa ajili ya kuwalipia wanafunzi gharama za matibabu wanapokwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya.
“Serikali yetu inawataka Watanzania wote wakiwamo wanafunzi kujiunga na mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili wawe na uhakika wa kutibiwa kwa wakati,ubora na kwa bei nafuu,nawaomba sana wazazi wenzangu hakikisheni mnawakatia Bima za afya watoto wenu”
Alisema,mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni shirika la umma lenye wajibu wa kuwahudumia Watanzania wote bila kubagua wakiwamo watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ambapo mzazi atatakiwa kujaza fomu zinazopatikana kwenye shule husika.
Kwa mujibu wa Hance,suala la matibabu kupitia mfuko wa Taifa wa Bima aya Afya ni jambo muhimu kwani hata tunapozungumzia suala la maendeleo haliwezi kupatikana kama watu hawatakuwa na afya njema.
Alisema,Wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma kwa jumla umebarikiwa kuwa na ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali na watu wanaofanya kazi kwa kujituma,hivyo sio rahisi wazazi kukosa fedha kwa ajili kuwaunganishwa watoto na NHIF.
Alisema, kwa kawaida mwanafunzi mwenye afya iliyotetereka hawezi kuwa msikivu darasani jambo linaloweza kumuathiri na kufanya vibaya katika masomo na mitihani yake kwa sababu atatumia muda wa masomo kwenda Hospitali au kukaa nyumbani.
Alisema,suala la Bima ya afya hasa kwa wanafunzi wanaokaa Bweni ni muhimu kwani litapunguza usumbufu kwa walimu kutumia fedha zao kuwalipia wanafunzi gharama za matibabu badala ya gharama hizo kubebwa na wazazi.
Aidha,ameupongeza uongozi wa shule ya Sekondari Kigonsera kwa kuweka utaratibu ambao unamtaka kila mwanafunzi anayejiunga na shule hiyo awe na kadi ya matibabu ya mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, mkakati uliosaidia sana wanafunzi wake kufanya vizuri kitaaluma.
Meneja huyo wa NHIF, amewashauri wazazi kupunguza matumizi yasio lazima ili kuwa na fedha ambazo zitatumika kuwalipia watoto wao kwenye mfuko huo na kusisitiza kuwa,NHIF itaendelea kuboresha huduma zake ili wanachama wafurahie huduma bora.
Amewaomba wazazi na jamii kwa jumla,kutoa ushirikiano kwa NHIF ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwani tangu ulipoanzishwa zaidi ya miaka 20 umeonesha mafanikio makubwa katika kuwahudumia watanzania.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo Ifgenia Nzota alisema, mara kwa mara wanapata usumbufu wa kuwaita wazazi kwenda kuwachukua watoto wao wanaoumwa ambao hawana bima ya afya kwa ajili ya kuwapeleka Hospitali jambo linalochangia baadhi ya watoto hao kukosa vipindi darasani.
Alisema,kama wazazi watawalipia watoto bima ya afya kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza baadhi ya gharama ikiwamo matibabu na nauli ya kwenda shuleni na kurudi nyumbani.
Nzota amewasisitiza wazazi kuhakikisha wanawaruhusu watoto kurudi shuleni mapema mara baada ya kupata matibabu, badala ya kukaa nyumbani kwa muda mrefu huku wakiendelea kupitwa na masomo.
MWISHO.