Ataka wenye ulemavu kutofichwa, washirikishwe katika maendeleo ya Taifa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, amewataka wazazi na walezi wasiwafiche watoto wenye ulemavu na wahakikishe wanafahamika mahali walipo, hali zao za ulemavu ili waweze kupata huduma stahiki na washiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 25, 2025), wakati akizindua Kanzidata na Mfumo wa Taarifa za Watu Wenye Ulemavu unaotokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amezitaka taasisi zote zinazotoa huduma kwa watu wenye ulemavu watumie takwimu hizo katika kutayarisha programu za kuwawezesha na kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo kujiendeleza kiuchumi, kijamii na mazingira.
“Taasisi zote za umma, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo washirikiane na Serikali kutumia mfumo huo kikamilifu kwa kufanya maamuzi yenye vigezo vya kitakwimu katika kupanga na kufuatilia utekelezaji wa sera, mipango na afua mbalimbali zinazolenga kukuza na kuimarisha maendeleo ya watu wenye ulemavu.”
Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote nchini wahakikishe Ofisi za Ustawi wa Jamii katika halmashauri zote nchini zinatekeleza wajibu wa kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi wenye ulemavu,. “Watekelezaji na wasimamizi wa miradi mbalimbali ya ujenzi wahakikishe uwepo wa miundombinu fikivu kwa ajili ya watu wenye ulemavu.”
Akizungumzia kuhusu matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, amesema asilimia 11.2 ya watu wote nchini wana ulemavu wa aina fulani, idadi hiyo imeongezeka kutoka asilimia 9.3 ilivyokuwa katika Sensa ya Mwaka 2012.
Akielezea kuhusu juhudi za kuimarisha ustawi wa watu wenye ulemavu nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha ustawi bora wa jamii ya watu wenye ulemavu ikiwemo kutunga na kutekeleza sera, sheria na programu mbalimbali za kulinda haki, fursa na maendeleo ya Watu wenye Ulemavu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande amesema matokeo hayo ni nyenzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya wizara yanayolenga kukuza maendeleo ya watu wenye ulemavu.
“Tumeshuhudia namna ambavyo kumekuwa na ongezeko la matumizi ya takwimu katika kupanga na kutekeleza shughuli zetu za Serikali ikiwemo upangaji wa bajeti za kisekta na bajeti kuu ya Serikali.
Nitoe wito kwa wizara, idara, taasisi za wakala wa Serikali kuhakikisha wanatumia matokeo haya tunayoyazindua leo pamoja na takwimu nyingine rasmi ili kuhakikisha kuwa bajeti ya mwaka 2025/2026 inaakisi kikamilifu mahitaji halisi ya watu wenye ulemavu.”
Naye, Mwakilishi Msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) Tanzania, Dkt. Majaliwa Marwa amesema shirika hilo linatoa wito kwa wadau na washirika wa maendeleo, asasi za kiaraia, sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kutumia takwimu na taarifa hizo ili kupanga na kufanya maamuzi kwa ustawi wa jamii nzima katika dhana ya kutomuacha mtu nyuma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA), Mwadawa Khamisi ameiomba Serikali ifanye utafiti wa kubaini vitu vinavyosababisha ongezeko la watu wenye ulemavu nchini ili iweze kukabiliana navyo kwa kushirikiana na wadau.
Pia, Mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa uongozi wao bora, imara na mstari wa mbele kwa kutetea watu wenye ulemavu.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Tungi Mwanjala amesema taarifa hizo zitaisaidia Serikali kuandaa mipango mbalimbali itakayoleta ujumuishi katika utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu.