Home BUSINESS WIZARA YA FEDHA YAWAHAKIKISHA WANANCHI ELIMU YA FEDHA

WIZARA YA FEDHA YAWAHAKIKISHA WANANCHI ELIMU YA FEDHA

Mratibu wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha, Halmashauri ya Jiji la Arusha, Bi. Fatuma Amiri, akizungumza na wananchi wa Kata ya Murieti katika Shule ya Msingi Msasani jijini Arusha, wakati wa kuikaribisha Timu ya Wataalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha, iliyoambatana na Maafisa kutoka taasisi na wadau mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa wajasiriamali na wananchi wa Mkoa wa Arusha.

Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, akitoa ufafanuzi kuhusu filamu ya elimu ya fedha kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa Kata ya Murieti, jijini Arusha, waliofika katika Shule ya Msingi Msasani kwa ajili ya kupata elimu ya fedha, ikiwa ni awamu ya tatu ambapo Wizara ya Fedha inalenga kutoa elimu hiyo kwa wananchi wote nchini.

Baadhi ya wajasiriamali na wananchi wa Kata ya Murieti wakipata elimu ya fedha katika Shule ya Msingi Msasani jijini Arusha, kwa njia ya filamu yenye maudhui kuhusu matumizi sahihi ya fedha, umuhimu wa kupanga bajeti na kuitekeleza, umuhimu wa kusajili vikundi vya huduma ndogo za fedha, utunzaji wa fedha binafsi, umuhimu wa kushirikisha familia na watu wa karibu kwenye masuala ya fedha na uwekezaji, umuhimu wa kukata bima ya biashara na mali nyingine, filamu hiyo imeandaliwa na Wizara ya Fedha lengo likiwa ni kusambaza elimu ya fedha kwa njia rahisi ya burudani ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa masuala ya huduma za fedha.

Mchumi kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Godfrey Mwatwinza, akitoa elimu ya fedha kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa Kata ya Murieti katika Shule ya Msingi Msasani, Jiji la Arusha kuhusu masuala ya uwekezaji, utunzaji wa fedha binafsi, kuweka akiba, kusajili vikundi vidogo vya fedha pamoja na masuala ya mikopo ikiwa ni Awamu ya Tatu ya Mafunzo ya Elimu ya Fedha yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Fedha.

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), mkoani Arusha, Bw. Josephat Komba, akieleza faida za wajasiriamali kujiunga na Mfuko huo, baada ya wajasiriamali hao kujitokeza katika viwanja vya Shule ya Msingi Msasani jijini Arusha kwa ajili ya kupata elimu ya fedha kutoka kwa Wataalam kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali alipoungana na Timu hiyo ya wataalam kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Maafisa kutoka taasisi na wadau mbalimbali.  

 Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF- Arusha.

Na Asia Singano, WF- Arusha

Serikali kupitia Wizara ya Fedha, imeahidi kuendelea kutekeleza azma yake ya kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wananchi wote ili kuhakikisha kuwa wanaelimika kuhusu masuala ya fedha, mikopo, uwekezaji ili kuwawezesha wananchi kutumia huduma sahihi za fedha.

Akizungumza jijini Arusha, Afisa Mwandamizi, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, wakati akitoa elimu ya fedha kwa wajasiliamali na wananchi wa Mtaa wa Muriet jijini Arusha, alisema Wizara iliona umuhimu wa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wote ili kuwajengea nidhamu ya matumizi ya fedha.

Bw. Kimaro alisema kuwa wananchi wengi wanashindwa kupiga hatua kiuchumi kutokana na uelewa mdogo juu ya matumizi sahihi ya fedha, kukosa usimamizi mzuri wa fedha zao pamoja na kutokuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba na kuwekeza hali inayosababisha baadhi ya wananchi fedha wanazopata kutobadilisha maisha yao kiuchumi.

“Imekuwa ni kawaida kusikia vilio vya wananchi wakiwa wamepata changamoto za mikopo wanakopa kwa watu wasio rasmi kutokana na kukosa uelewa wa wapi wanapaswa kukopa na namna ya kutumia hiyo mikopo jambo linalowaletea madhara” alisema Bw. Kimaro

Akitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya uwekezaji, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoani Arusha, Bw. Josephat Komba, aliwataka wajasiriamali kuwekeza sehemu sahihi ili kuepuka kupoteza fedha zao.

‘’Nawasihi kuwekeza kwenye maeneo ambayo fedha zenu zitakuwa salama na mtapata faida, karibuni kuwekeza NSSSF, kwakuwa kwa kila kiasi cha fedha zako unachoweka utapata akiba na utapata bima ya afya’’ alisema Bw. Komba.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Muriet, Bw. Rashid Juma, aliwataka watoa huduma za fedha katika mtaa huo kufuata sheria na taratibu za huduma ndogo za fedha kama mafunzo yalivyotolewa na timu ya wataalam wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha.

‘’Natoa onyo kwa watoa mikopo mtaani kwangu, ni marufuku kumfuata mtu usiku wa manane kudai pesa, wengine wanaingia kwenye matatizo wanaitiwa wezi wanapigwa kumbe sio wezi wameenda kudai mikopo, kopesheni kwa kufuata taratibu zilizowekwa’’ alisema Bw. Juma.

Hii ni Awamu ya Tatu ya Elimu ya Fedha inayotolewa na Wizara ya Fedha, ambapo kwa awamu hii mikoa mbalimbali inatarajiwa kufikiwa ikiwemo mkoa wa Arusha ambapo imeanza kutolewa huku mikoa mingine ikiwa ni Kilimanjaro, Mwanza pamoja na Mkoa wa Mara lengo likiwa ni kuwapa elimu wananchi kuhusu masuala ya fedha ikiwemo matumizi sahihi ya fedha binafsi, uwekaji akiba uwekezaji.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here