Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo akizungumza katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari kuelezea mafanikio katika sekta ya Uwekezaji nchini. Mkutano huo umefanyika leo Januari 10, 2025 Jijini Dar es Salaam.
PICHA NA; HUGHES DUGILO
NA; Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, amesema kuwa mwaka 2024 umevunja rekodi na kuweka historia katika sekta ya Uwekezaji nchini tangu kuanzisha kwake na kupata mafanikio makubwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC kwa kusajili jumla ya miradi 901, katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2024, ikilinganishwa na miradi 526 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Profesa Mkumbo amebainisha hayo katika mkutano na Wahariri na waandihi wa Habari uliofanyika leo Januari 10, 2025 Jijini Dar es Salaam ambapo amesema Miradi iliyosajiliwa mwaka jana inatarajiwa kuzalisha ajira 212,293 ikilinganishwa na ajira 137,010 zilizozalishwa na miradi ya uwekezaji katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Aidha, amesema miradi hiyo imevutia mtaji wa dola za kimarekani bilioni 9.31, ikilinganishwa na mtaji wa dola za Kimarekani bilioni 5.72 iliyotokana na miradi ya uwekezaji kupitia TIC katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2023.
’’Mwaka 2024 tunaweza kuutangaza kuwa mwaka bora zaidi katika sekta ya uwekezaji Tanzania kutokana na ukweli kwamba ndiyo mwaka ambao TIC kusajili miradi mingi zaidi ya uwekezaji (miradi 901) tangu Tanzania ianzishe kituo hiki na kuanza kurekodi miradi ya uwekezaji. Hii inavunja rekodi ya miradi 885 ya mwaka 2013. Hadi kufikia Disemba 2024, TIC ina miradi 13,282 ya uwekezaji iliyosajiliwa na kutekelezwa nchini, ikivutia mitaji kiasi cha dola za kimarekani 127,176 milioni na kutoa ajira zaidi milioni moja’’ amesema Profesa. Mkumbo.
Profesa Mkumbo ameongeza kuwa Serikali kwa mwaka 2025 itachukua hatua mbalimbali ikiwa ni Katika kuendelea kuimarisha sekta ya uwekezaji nchini, na kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kote nchini
Hatua hizo ni pamoja na Kutunga Muswada wa Sheria mpya ya Uwekezaji Tanzania. ambao unapendekeza kuunganisha taasisi za TIC na EPZA, uliowasilishwa Bungeni mwaka 2024 ambapo sasa upo katika ngazi ya Kamati ya Kudumu ya Bunge kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Amesema, hatua nyingine ni Kuandaa awamu ya pili ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI) ambao ulibaini mafanikio mbalimbali katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kubaini changamoto mpya zilizojitokeza ambazo serikali na wadau wameendelea kuzifanyia kazi kwa lengo la kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye mazingira bora ya kufanya biashara na uwekezaji barani Afrika.
Ameeleza kuwa, maeneo mengine ni kuanzisha utaratibu wa kuzipima Mamlaka za serikali za mitaa katika kuboresha mazingira ya biashara na kuhamasisha kuwezesha uwekezaji, Kuanza kutekeleza ujenzi wa miundombinu katika maeneo maalum ya kiuchumi ikiwemo la Bagamoyo (Bagamoyo Special Economic Zone) ili kuwezesha ujenzi wa viwanda. kushirikiana na watanzania waishio nje ya nchi (diaspora), kuanzisha utaratibu wa kuhamasisha uwekezaji kwa kuzingatia taratibu zitakazowekwa na TIC kwa kushirikiana na mamlaka zingine za serikali.
’’Mwaka 2025, tumejiwekea lengo la kuvutia miradi mipya 1,500 ya uwekezaji na mitaji ya dola za kimarekani bilioni 15 ifikapo Disemba 2025. Sekta mahususi ni viwanda, kilimo, uchukuzi, nishati safi, utalii, madini na huduma.
’’Ongezeko hili litaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi tano bora katika uwekezaji barani Afrika hasa kwa wingi wa mitaji. Kwa utoaji huduma, Tanzania ni moja ya nchi bora kwa uwekezaji hata sasa’’ amesema Profesa Mkumbo.