Home Uncategorized TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YACHUNGUZA VIFO VYA WATU...

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YACHUNGUZA VIFO VYA WATU WAWILI PEMBA

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeeleza kuwa inachunguza vifo vya watu wawili vilivyotokea hivi karibuni katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Januari 10, 2025, na Kamishna wa Tume hiyo Zanzibar, Khatib M. Mwinchande, tukio hilo limehusisha vifo vya Nd. Athuman Hamad Athuman (75) na Nd. Amour Khamis Salim (28), ambao walikuwa wakaazi wa kijiji cha Kiungoni, Wete, Pemba. Vifo hivyo vilitokea mwezi Desemba 2024, na Kamishna Mwinchande alitoa tamko hilo ofisini kwake, Mbweni, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Kamishna Mwinchande alieleza kuwa tukio la mauaji hayo ni ukiukwaji wa haki ya kuishi, kama ilivyoainishwa na Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 13(2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Tume hiyo imelaani vikali vitendo hivyo, ikisema ni kinyume na haki za msingi za binadamu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, iliyotolewa Desemba 25, 2024, marehemu walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ali Khamis Camp, Vitongoji, Pemba. Aidha, taarifa za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii zimeeleza kuwa marehemu walikamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa baiskeli na matumizi ya bangi, lakini walirudishwa wakiwa wamefariki siku iliyofuata.

Kamishna Mwinchande alieleza kuwa matukio hayo ni ukatili wa hali ya juu dhidi ya binadamu na yanakiuka Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kifungu cha 13(3) cha Katiba ya Zanzibar. Vilevile, tukio hilo limekiuka haki ya uhuru wa kuishi kama mtu huru, kama inavyoainishwa katika Ibara ya 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kamishna huyo alibainisha kuwa mauaji hayo yametokea wakati Tume ikiwa bado inafuatilia matukio ya mauaji mengine kama vile yale ya Kidoti, Kaskazini Unguja, pamoja na matukio ya aina hiyo Tanzania Bara.

THBUB imeahidi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hili na matukio mengine yanayofanana nalo ili kuimarisha misingi ya utawala bora na utawala wa sheria nchini. Kamishna Mwinchande ametoa wito kwa wananchi na taasisi zinazohusika kushirikiana na Tume na vyombo vingine vya uchunguzi ili kuhakikisha haki inatendeka.

Aidha, Tume imesisitiza umuhimu wa jamii kupiga vita vitendo vyote vya ukiukwaji wa sheria, haki za binadamu, na misingi ya utawala wa sheria.

Kamishna Mwinchande ametoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, na marafiki wa marehemu Athuman Hamad Athuman na Amour Khamis Salim kwa msiba mzito wa kupoteza wapendwa wao kwa njia hiyo ya kusikitisha. Pia amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi unaendelea. 

Marehemu walikuwa wakaazi wa Kimango, Kiungoni, Wete, Pemba, na vifo vyao vimeibua maswali mengi kuhusu utekelezaji wa haki na sheria. THBUB imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia misingi ya haki na sheria ili kuzuia matukio ya aina hii kutokea tena.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here