Na.Majid Abdulkarim – WAF
Matibabu ya Ugonjwa wa Fistula kwa sasa yanapatikana katika Hospital zote za Mikoa nchini ambapo awali matibabu hayo yalikuwa yakipatika katika Hospitali ya CCBRT pekee na ugonjwa huo unatibika.
Kauli hiyo imebainishwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa mahojiano katika kipindi cha Sentro kinachorushwa kupitia Televisheni ya Clouds.
Waziri Ummy amesema ugonjwa wa Fistula ni ugonjwa ambao unawakumba wanawake na kuwafanya kutokwa na mkojo dakika yoyote bila wao kujua hivyo kusababisha harufu kali na kupelekea baadhi ya watu kuwanyanyapaa.
“Kwa Sasa ukubwa wa tatizo hili wanawake 3,000 hupata matatizo hayo kwa mwaka, Fistula husababishwa na uchungu pingamizi yaani mtu kama anataka kujifungua na mtoto hatoki, kunakuwa na msukumo na wengine wanakuwa mbali na vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na hospitali.” amesema Waziri Ummy
Hata hivyo Waziri Ummy alisema hatua zisipochukuliwa mapema mama akipata uzazi pingamizi ndani ya muda wa masaa 48 mpaka 72 ndo anaweza kupata ugonjwa wa Fistula.
Katika kukabiliana na ugonjwa huo Waziri Ummy alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeweka mkakati wa kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto ikiwemo huduma za uzazi.
“Hapa kazi kubwa alofanya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha ameboresha huduma za akina mama wajawazito kwa kuhakikisha wanawake wanaopata uzazi pingamizi wanapata huduma za upasuaji katika vituo vya kutolea huduma za afya na hospitalini”, ameweka wazi Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameendelea kwa kuwahimiza wanawake wajawazito kuhudhuri kliniki mapema kama ambavyo wataalamu wanashauri kuhudhuria maadhurio manne kwa muda wa ujauzito wao ili kujua maendeleo ya ujauzito.
Pia ametoa rai kwa jamii kuwasaidia wajawazito kuwahi vituoni kupata huduma mapema ambapo amesema walizindua mpango wa M-Mama wa kusaidia kufika vituoni haraka kwa kuwa changamoto kubwa ni usafiri.
Huduma ya M-Mama chini ya Ufadhili wa Vodacom itawezesha wajawazito kupata usafiri wa kuwahi kufika hospitali.
MWISHO