Home BUSINESS MSAADA PEKEE KWA WAKULIMA WA TANZANIA NI KUONGEZA VIWANDA VYA KUSINDIKA MAZAO...

MSAADA PEKEE KWA WAKULIMA WA TANZANIA NI KUONGEZA VIWANDA VYA KUSINDIKA MAZAO PAMOJA NA UHAKIKA WA MASOKO – PROF. MKENDA

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Mgeni wake Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright Ofisini kwake Jengo la Kilimo IV Jijini Dodoma leo tarehe 16 Juni, 2021.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akimsikiliza Mgeni wake Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright Ofisini kwake Jengo la Kilimo IV Jijini Dodoma katika mazungumzo hayo Waziri Mkenda amemueleza Mgeni wake kuwa Tanzania bado  inahitaji Wawekezaji zaidi kwenye Sekta ya Kilimo hususan kwenye mazao ya mbegu za mafuta pamoja na mazao ya mboga na matunda (Horticultural Crops).

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akimkabidhi Mgeni wake Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright zawadi ya korosho za Tanzania mara baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisini kwake Jengo la Kilimo IV Jijini Dodoma leo tarehe 16 Juni, 2021.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akipokea zawadi ya kitabu cha Texas Hill Country kutoka kwa Mgeni wake Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright; Kitabu cha Texas Hill Country kinaelezea taarifa mbalimbali kuhusu utalii na mambo mbalimbali kuhusu Jimbo la Texas.

 

DODOMA.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amemwambia Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright kuwa Wakulima wa Tanzania wanahitaji uhakika wa masoko ya mazao ya kilimo pamoja na ujenzi wa viwanda vya kusindika na kuongeza thamani mazao ya kilimo kutoka kwa Wawekezaji wa nchini Marekani na kwamba Wizara ipo tayari kuratibu mkutano na Wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka Marekani ili waje nchini kwa ajili ya kuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo.

Waziri Mkenda amemueleza Balozi Dkt. Wright leo mchana tarehe 16 Juni ofisini kwake Jijini Dodoma kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imefanya juhudi za makusudi kuhakikisha kilimo cha Tanzania kinakuwa chenye tija zaidi na cha kumuinua Mkulima.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa bajeti ya Sekta ya Kilimo kwenye eneo la uzalishaji wa mbegu bora za alizeti imeongezeka mara dufu ili kuongeza uzalishaji wa alizeti kama njia mojawapo ya kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi ambapo taifa hutumia zaidi ya shilingi bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. 

Waziri Mkenda alisema Wizara ya Kilimo imeweka mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji na tija kwenye mazao ya mafuta. Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za mazao ya mafuta.

“Katika mwaka 2021/2022 Serikali imeongeza bajeti ya Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) kutoka shilingi bilioni 7 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11 mwaka 2021/2022 sambamba na hilo bajeti ya Wakala wa Mbegu wa Kilimo (ASA) imeongezeka kutoka bilioni 5 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 10 mwaka 2021/2022 ili kuongeza upatikanaji wa mbegu bora zikiwemo mbegu za mazao ya mafuta.” Amekaririwa Prof. Mkenda.

Waziri Mkenda ameutaja mkakati mwengine ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani; ambapo Wizara itaendelea kuimarisha huduma za ugani kwa kuwapatia vyombo ya usafiri maafisa ugani ikiwemo kununua pikipiki 1,500, vifaa maalum vya kupimia udongo (Soil Test Kits), visanduku vya ugani (Extension Kits), simu janja na kuwezesha uanzishaji wa mashamba ya mfano kwa kila afisa ugani na kutoa mafunzo rejea.

“Huduma hizo zitawezeshwa kwa kuwa Wizara imeongeza bajeti ya Kuimairisha huduma za ugani kutoka Shilingi milioni 603 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11 mwaka 2021/2022. Katika utekelezaji wa mpango huo, Wizara imechagua Mikoa mitatu ya kielelezo; Mikoa hiyo ni Singida, Dodoma na Simiyu yenye fursa kubwa ya kuzalisha mazao ya mafuta hususan alizeti na pamba.” Amekaririwa Prof. Mkenda.

Mkakati mwengine ni pamoja na kuhamasisha uanzishaji wa mashamba ya pamoja na kuimarisha kilimo cha mkataba.

“Wizara itaendelea kuhamasisha uanzishaji wa mashamba ya pamoja (block farming) katika mikoa inayozalisha mazao ya mafuta kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo mbegu bora, mbolea, viuatilifu na zana bora za kilimo pamoja na mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima.”

“Aidha, Serikali itaimarisha kilimo cha mkataba kwa mazao ya mafuta kwa lengo la kuwa na uhakika wa masoko”. Alisisitiza Waziri Mkenda.

Kwa upande Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright amesema Marekani na Tazania zinahusiano mzuri na wa muda mrefu na kwamba itaendelea kushirikiana na Tanzaniua katika Sekta ya Kilimo Mazao na kuahidi kuwa ubalozi utatoa msaada kwa kila hitaji litakalokuwa ndani ya uwezo wa Taifa lake.

 

 

Previous articleDKT. GWAJIMA AZUNGUMZA NA SHIRIKA LA PCI.
Next articleBUPE MWAKANG’ATA ALIA NA MATUTA BARABARANI SONGWE, TUNDUMA KWENDA SUMBAWANGA MJINI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here