Home BUSINESS IFIKAPO 2030 KOROSHO ZOTE ZITABANGULIWA NCHINI – BASHE

IFIKAPO 2030 KOROSHO ZOTE ZITABANGULIWA NCHINI – BASHE

Na MWANDISHI WETU,

WAZIRI WA KILIMO Mhe. Hussein Bashe, (Mb) amesema ujenzi wa Kongani ya Viwanda Maranje Newala mkoani Mtwara unalenga kuhakikisha ifikapo 2030, korosho zote zinabanguliwa nchini.

Amesema, lengo ni kuhakikisha wakulima hawauzi korosho ghafi nje ya nchi.

Bashe amesema hayo katika muendelezo wa ziara yake Mkoani Mtwara, wakati akizindua kiwanda cha kubangua Korosho cha TANECU kilichopo katika kijiji cha Mmovo, kata ya Kitangali Halmashauri ya Newala mkoani Mtwara

Amesema, kiwanda hicho kilicho gharimu zaidi ya sh. Bilioni 3.4 kimelenga kufungua milango ya ujenzi wa mradi wa kongani ya viwanda Newala ambapo hadi kufikia mwaka 2030 korosho zote zitabanguliwa nchini.

Kiwanda hicho ni moja kati ya viwanda/Kongani kumi vitakavyojengwa katika eneo lenye mita za mraba 99,000.

Uwezo wa kiwanda kimoja ni kubangua tani 3,500 za korosho ghafi kwa mwaka.

Ametumia fursa hiyo kuutaka Ushirika nchini kubadili mfumo wake wa uendeshaji na kuzingatia mahitaji ya wakulima.

Waziri Bashe amesema anatambua kuwa taswira ya vyama vya ushirika nchini imebadilika kwani miaka michache iliyopita, vyama hivyo vilikuwa na madeni kila kona.

Pia, Bashe ameeleza mipango ya Serikali kufungua kiwanda kingine cha kuchakata tani 3,000 za Korosho Tandahimba ifikapo mwanzo wa Msimu wa mavuno 2025.

“Naomba kusisitiza kuwa, kabla ya mwisho wa mwaka huu,mizani ya kidigitali pia itakuwa imekamilika tayari kwa kuanza kazi,”amesema.

Waziri Bashe ameeleza kuwa mpango wa serikali kuendelea kushirikiana na Bodi ya Korosho kuajiri maafisa ugani 400 mkoani humo ambao watashirikiana na vyama vya msingi vijijini kuandaa taarifa za wakulima na kusaidia kukua kwa sekta upo palepale.

      

Previous articleWATAALAMU WA MAABARA TOENI MAJIBU SAHIHI KUWASAIDIA WATANZANIA – DKT. BITEKO
Next articleKITUO CHA AFYA SUMBAWANGA  KUHUDUMIA WANANCHI ZAIDI YA HAMSINI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here