Home LOCAL KABATI AWATAKA WANAWAKE KUCHANGAMKIA FURSA YA KILIMO CHA MATUNDA NA MBOGAMBOGA

KABATI AWATAKA WANAWAKE KUCHANGAMKIA FURSA YA KILIMO CHA MATUNDA NA MBOGAMBOGA

Na: Khalfan Akida, IRINGA.
Wanawake mkoani Iringa wametakiwa kuchangamkia fursa itokanayo na uhitaji mkubwa wa mazao ya kilimo cha mbogamboga na matunda Duniani kwa sasa.

“Soko la Dunia sasa hivi linauhaba mkubwa wa mazao ya kilimo hasa matunda na mboga mboga, na hii ni fursa ambayo wanawake tunatakiwa kuitumia Iringa”

Hayo yamesemwa leo na Dkt. Ritta Kabati (Mb)  katika baraza la Jumuiya ya Umoja wa Wanawake w Chama Cha Mapinduzi Katika wilaya ya Kilolo, Mkoani Iringa lililofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya mkuu wa Wilaya.

Kabati amesema kutokana na uhitaji mkubwa wa mazao ya mbogamboga na matunda wanawake wanapaswa kutumia upungufu huo kujiingiza katika kilimo na kuhakikisha wanazalisha kitaalamu ili kujipatia kipato.

Kabati amesisitiza uwepo wa mazingira rafiki yaliyowekwa na serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa wafanyabiashara na wakulima na pia serikali iko mbioni kuleta ndege itakayotumika kusafirisha mizigo ikiwemo mazao ya Kilimo.”ndege inakuja ya kubebea mizigo itakuwa rahisi tu kwa wakulima na wafanyabiashara, lakini pia serikali imeweka sheria na mikakati mizuri kusaidia wakulima”

Kwa upande wake, Katibu wa UWT mkoa wa Iringa, Angela Milembe amewataka wanawake wajiunge katika vikundi vya ujasiriamali ikiwemo kilimo ili kupatiwa mafunzo na mitaji ya kuendeshea shughuli zao.

“Niwahamasishe mkajiunge vikundi kama bado hamjajiunga ili mpatiwe mafunzo pamoja na mitaji midogo dogo ya kuanzisha shughuli zenu.”

Bi. milembe amesema mkoa wa Iringa unafursa kubwa ya kuwepo kwa hali ya hewa inayostawisha mazao ya aina mbalimbali yenye uhitaji mkubwa kwa sasa katika soko la Dunia na hivyo ni muhimu kwa Wanawake kujiingiza katika fursa hiyo ya Kilimo. “Iringa kuna hali ya hewa nzuri na udongo mzuri unaokubali mazao ya aina mbalimbali, hivyo wanawake sasa tujikite katika kilimo cha matunda, yana soko sana sasa”

Nao wanawake watokanao na Jumuiya ya UWT wilayani Kilolo wameahidi kuanzisha mashamba ya mfano yatakayojikita katika kilimo zaidi katika kilimo cha matunda na mboga mboga huku wakisisitiza zaidi kupatiwa elimu ya kilimo hicho.
Previous articleWAZIRI MKUU AWASILI NCHINI MOROCCO KWA ZIARA YA KIKAZI
Next articleWAZIRI GWAJIMA AWATAKA WAHUDUMU WA AFYA NCHINI KUWA WAKARIMU

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here