Imeelezwa kuwa Jamii ya watanzania hususani vijana wanaweza kupata fursa ya kujiajiri wenyewe na kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa kujiendeleza kimasomo katika nyanja ya usafirishaji kutokana na Sekta hiyo kuwa na umuhimu mkubwa kwenye jamii.
Hayo yameelezwa na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Tulizo Chusi alipokuwa kwenye mahojiano na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) katika viwanja vya mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam ambapo wanafunzi na wadau mbalimbali wa Elimu wamepata fursa ya kutembelea chuo hicho kufahamu kozi zinazotolewa na chuo hicho na kuweza kufanya Udahili wa papo hapo.
Chusi amesema kuwa Sekta ya usafirishaji ina umuhimu mkubwa hasa katika kuendeleza na kuimarisha Sera ya uchumi wa Viwanda nakwamba fani mojawapo inayotolewa kwenye chuo ni ya Logistics na usafirishaji ambapo wanafunzi wanafunzi wanaohitimu kwenye fani hizo wanaweza kufanyakazi kwenye viwanda mbalimbali na kuongeza tija katika uzalishaji.
“kwenye viwanda kuna uhitaji wa Logistics na usafirishaji hivyo kozi hiyo inaweza kusaidi kuendeleza Sekta hiyo, pia tuna kozi za Reli inaweza kusaidia kwenye mambo ya SGR na hii pia ni muhimu sana kwenye kukuza uchumi wa viwanda kwa hivyo tuna kozi nyingi sana ambazo mtu akisoma anaweza kujiajiri mwenyewe na kuweza kufanyakazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye Sekata ya viwanda”
“Wanafunzi wote tunawakaribisha sana waweze kufika hapa kwenye Banda letu, lakini pia wanaweza wakatupata kupitia Website yetu ambayo ni www.nit.ac.tz ambapo pia wanaweza kufanya udahili lakini hata wakifika hapa kwenye Banda letu tunawasajili hapa hapa na kuweza kujiunga na chuo chetu” Amesema Tulizo.
Maonesho hayo ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yenye kaulimbiu “Kuendelea Kukuza na Kudumisha Uchumi wa Kati kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia”. yanafanyika kwa siku sita katika viwanja vya mnazi mmoja Dar es Salaam na kufikia kilele chake siku ya J.mosi Julai 31,2021.