Home BUSINESS MANALA AIOMBA SERIKALI KUJENGA UWANJA WA NDEGE KAHAMA

MANALA AIOMBA SERIKALI KUJENGA UWANJA WA NDEGE KAHAMA

Barua ya Wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan 
Kupitia Waziri wa Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi
 
Mhe. Rais,
 
YAH: OMBI LA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE KATIKA MANISPAA YA KAHAMA
 
Kwa heshima na taadhima, napenda kuchukua nafasi hii kukupongeza Mhe. Rais kwa kazi kubwa na nzuri inayoendelea kufanyika chini ya uongozi wako thabiti. Nikiwa mwananchi na mdau wa maendeleo katika Manispaa ya Kahama, napenda kuwasilisha ombi langu la kujenga uwanja wa ndege ndani ya manispaa hii muhimu, ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii katika eneo hili na nchi kwa ujumla.
 
Manispaa ya Kahama, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, inakadiriwa kuwa na idadi ya watu takribani milioni 1. Hii inaashiria kwamba nusu ya wakazi wa Wilaya ya Kahama wanatoka ndani ya manispaa hii. Ukosefu wa uwanja wa ndege katika eneo hili umekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na usafirishaji wa haraka wa abiria na mizigo. Watu wengi wanakosa huduma hii muhimu, hali inayosababisha gharama kubwa za usafiri na muda mwingi kwa wakazi wa Kahama na maeneo jirani wanapotumia viwanja vya ndege vya Shinyanga au Mwanza.
 
Kahama ni miongoni mwa wilaya zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika Pato la Taifa kupitia vitega uchumi mbalimbali kama vile madini, kilimo, na biashara. 
 
Uwepo wa uwanja wa ndege katika Manispaa ya Kahama utachochea zaidi ukuaji wa sekta hizi kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma, na kuongeza mapato ya serikali. Takwimu zinaonyesha kuwa uwepo wa uwanja wa ndege unaweza kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi kikubwa kupitia ada na kodi mbalimbali zinazohusiana na shughuli za usafiri wa anga.
 
Pamoja na faida hizo kwa serikali, wananchi, wafanyabiashara, na makundi mengine yatakayohusishwa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na huduma hii, watapata fursa za ajira, kuongezeka kwa usafirishaji wa bidhaa za kilimo, madini, na biashara, pamoja na kuboresha hali ya maisha kwa ujumla. Manispaa ya Kahama ikiwa na vitega uchumi vingi, mabadiliko haya yatakuwa na athari chanya kwa uchumi wa eneo hili na taifa kwa ujumla.
 
Iwapo utekelezaji wa mradi huu muhimu utachelewa kutokana na sababu mbalimbali, napendekeza hatua mbadala kama ifuatavyo:
 
1. Kutathmini na kupanua uwanja wa ndege wa Buzwagi: Uwanja huu ambao sasa ni mali ya serikali, unaweza kufanyiwa tathmini na kupanuliwa ili kukidhi mahitaji ya usafiri wa anga kwa Kahama na maeneo jirani.
 
2. Kupitia upya ratiba za ndege: Kupitia na kuongeza idadi ya siku za safari za ndege zinazotumia uwanja huo kwa wiki, ili kupunguza gharama kwa wakazi wa Kahama na maeneo jirani wanapolazimika kusafiri hadi Shinyanga au Mwanza kwa huduma hiyo.
 
Napenda kumalizia kwa kutoa pongezi kwa serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuendelea kutekeleza ahadi kwa Watanzania, wakiwemo wananchi wa Kahama.
 
 Naomba maombi yangu yaweze kupokelewa na kufanyiwa kazi kwa ajili ya maendeleo ya Manispaa ya Kahama na taifa kwa ujumla.
 
Nakutakia kazi njema na utekelezaji wa majukumu yenu kwa maslahi ya Watanzania wote.
 
Wako katika ujenzi wa taifa,
Mhandisi Dkt. Manala Tabu Mbumba  
Mdau wa Maendeleo Kahama
Previous articleEWURA YATETA NA MAJAJI,MAHAKIMU KUHUSU UDHIBITI
Next articleKATIBU MKUU WA CCM Dkt. NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE KINANA NYUMBANI KWAKE DSM
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here