Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Katika kuhakikisha wataalamu mbalimbali katika sekta ya Gesi na Mafuta ambao ni wazawa wanapata fursa ya ajira katika sekta hizo, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa juu wa Petroli (Pura) imesema kuwa imeshirikiana na Mamlaka ya Udhibiti na Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuandaa kazindata ya kusaidia na kuwatambua wataalam mbalimbali wa sekta hiyo kupata ajira kwa urahisi zaidi.
Mkuu wa kitengo Cha ushirikishwaji Wazawa na Uhusishaji wa Wadau kutoka katika Mamlaka hiyo Charles Nyangi amesema kuwa kazindata hiyo tayari imeanza kufanya kazi kuanzia mwezi mei mwaka huu 2022, kwa kuandikisha wataalamu hao kupitia tovuti ya Mamlaka hiyo na kwamba hiyo inatoa fursa kwa watanzania kuweza kutambulika kwa haraka na kuchangamkia fursa.
“Nipende kuwatangazia rasmi kuwa kupitia fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya Gesi na Mafuta tumeanzisha kazindata kwa kushirikiana na EWURA kuandaa wataalamu na kuwatambua kiurahisi pindi ajira zinapopatikana, ili waweze kushiri katika ajira hizo kupitia website yetu” alisema.
Pia Nyangi ameongeza kwa kuzungumzia ushiriki wao kwenye Maonyesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba ambapo amesema kuwa ushiriki wao kwenye maonesho hayo unatoa fursa kwa wananchi kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka hiyo hususani katika utafutaji, uchumbaji na usambazaji wa Gesi na Petroli.
“Tupo kwenye maonesho haya kwaajili ya kutoa elimu na kuwajengea uelewa wananchi kuhusu fursa zinazopatikana nchini katika eneo la gesi na mafuta na namna ambavyo wananchi wanaweza kutumia kanzidata kuzitambua fursa mbalimbali za Mafuta na gesi asilia zilizopo hapa.” ameongeza Nyangi.
Aidha ametoa mwito kwa jamii kujitoleza kwa wingi katika Maonesho hayo na kufika kwenye banda lao kujifunza na kuona fursa mbalimbali zinazopatikana katika taasisi yao.
Mwisho.