Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi (TRA) Richard Kayombo amesema kuwa, uongozi wa mamlaka hiyo umedhamiria kuwatumikia wananchi na kuyatekeleza maagizo yote aliyoyatoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ili kukusanya mapato kwa Serikali.
Kauli hiyo ameitoa mapema leo Septemba 3,2021 jijini Dar es Saalam wakati akifungua semina kwa Klabu ya waandishi wa habari wa jiji la Dar es Salaam (DCPC) iliyoandaliwa na Mamlaka hiyo lengo likiwa ni kufikisha elimu kwa umma kupitia waandishi wa habari kuhusu mabadiliko ya Sheria za kodi kwa 2021.
Kayombo amesema, kati ya maagizo aliyoyatoa Rais Samia ni pamoja na ukusanyaji wa kodi kwa haki pamoja na kupanua zaidi wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Amesema TRA imekuwa ikifanya ushirikishaji wa aina mbalimbali kwa wananchi kwa lengo la kukusanya mapato kwa kuzingatia weledi, haki pamoja na kusimamia kazi zake kwa weledi ili kufikia lengo la kukusanya kiwango cha Sh Trill 22.88 ambacho kimeelekezwa na Serikali.
Ameongeza kuwa, uboreshaji huo umehusisha pia mashine za kielektroniki (EFD’s) ambazo awali zililamikiwa sana na wafanyabiashara na kusababisha kuwapo kwa risiti za kughushi mitaani.
“Tumejipanga kuwatumikia wananchi, tumeandaa mpango mkakati wa uwajibikaji, weledi pamoja na uadilifu ambapo pia tumeanzisha utaratibu wa mnada katika mitandao, lengo ni kuongeza ufanisi, ushiriki katika kuleta ushindani wa haki pamoja na kufanya maboresho”amesema Kayombo.
Aidha amesema kutokana na kuwapo kwa wimbi la Ugonjwa wa Virusi vya COVID 19, TRA imefanikiwa kuanzisha huduma kwa njia ya mtandao kama njia ya kuepuka misongamano katika Ofisi za Mamlaka hiyo na kujikinga na maradhi hayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa DCPC), Irene Mark amesema klabu hiyo imekuwa ikifanyakazi kwa karibu na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo TRA lengo ni kutoa taarifa sahihi kwa wananchi baada ya waandishi hao kupatiwa mafunzo.
“DCPC imekuwa mdau mkuu wa taasisi mbalimbali ikiwamo TRA, lengo ni kuwezesha waandishi kufikisha ujumbe na taarifa sahihi kwa wananchi.
“Aidha tumekuwa mstari wa mbele kuisaidia Serikalini katika kupambana na ugonjwa wa korona kwa kuhamasisha umma kupata chanjo tukuwemo sisi wenyewe” amesema Iren.