Waziri wa madini Dkt Dotto Biteko akiongea na wafanyabiashara wa madini katika kikao chao kilichofanyika mji mdogo wa Mererani.
Katikati kulia ni waziri wa madini Dkt Dotto Biteko akiongea na mkuu wa mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere, kushoto ni mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka na kulia ni mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa madini (TAMIDA) Sammy Mollel
Wafanyabiashara wa madini wakiwa katika kikao chao na waziri wa madini kilichofanyika katika mji mdogo wa Mererani mkoani Manyara
NA: NAMNYAK KIVUYO, MANYARA.
Waziri wa madini Dkt Dotto Biteko amesema kuwa suala la wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite kuhamishia biashara hiyo katika eneo la Mererani ambapo ndipo madini hayo yanapopatikana hakuna anayeweza kupinga wala kufuta hivyo wafanyabiashara wahamie katika eneo hilo kwani changamoto zilizopo zitaendelea kuimarika polepole.
Dkt Biteko aliyasema hayo katika kikao chake kilichowajumuisha wafanyabiashara wa madini hayo wakiwemo Dillars, Brokers, na wachimbaji ambapo alisema kuwa wafanyanyabiashara waendelee kuhamia katika eneo hilo na polepole litahimarika na kukidhi mahitaji yao.
Alisema hajapuuza uwekezaji walioufanya Arusha kwani bado itaendelea kuwa kituo cha biashara kwani hakuna dhambi madini mengine kutoka nchi mbalimbali yakiendelea kuuzwa katika mkoa huo na Tanzanite ikauzwa Mererani.
“Biashara ya Tanzanite kuja Mererani sio jambo jipya lilianza tangu ujenzi wa ukuta kulizunguka eneo la machimbo lilipoanza na hatuta rudi nyuma kwenye haya maelekezo lakini tunajua kuna changamoto ila zitapata ufumbuzi wakati mmeshahamishia biashara zenu huku ,” Alisema Dkt Biteko.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere alieleza kuwa serikali ilishaamua hivyo wafanyabiashara hawana chaguo ambaye atashindwa kuhamia Mererani muda ukiisha anyimwe leseni kwani siku 90 zinatosha kudhibitisha ambao wataweza kuhamia na ambao watashindwa ambapo alisema hadi hivi sasa wafanyabiashara zaidi ya 50 wameshafungua ofisi katika eneo hilo.
Naye mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher ole Sendeka aliwasihi wafanyabiashara kuendelea kuhamia katika eneo hilo ili kuinua uchumi wa Mererani na istoshe agizo hilo limetolewa na Rais na hakuna mtu yoyote anayeweza kupinga hivyo wasijidanganye kuwa biashara ya Tanzanite itaendelea kufanyika Arusha.
“Nimesikia mmesema hakuna miundombinu ya kufungua ofisi katika eneo hilo kutokana na wingi wenu na vigozo vinavyotakiwa ili kufungua ofisi hizo hapa lakini kila kitu ni taratibu kwa sasa njooni kwenye hizi nyumba muendelee na biashara hadi hapo halmashauri itakapojenga jengo kwaajili ya biashara hii na mimi nitaendelea kuweka msukumo ili fedha za ujenzi zije,” Alisema Ole Sendeka.
Aidha kwa upande wa mmoja wa wachimbaji aliyejitambulisha kwa jina la Money Yusuph alisema kuwa wamewekeza sana katika uchimbaji wa Tanzanite kwa miaka mingi lakini cha ajabu thamani ya madini hayo inaendelea kushuka hivyo serikali iangali namna ya kuwaweka huru kwani wanabanwa sana ndio mana wanunuzi wananunua bei wanayotaka.
“Angalieni presha iliyopo mnatubana sana na hii haitusaidii wachimbaji bali inatuumiza, tusaidiane kuiokoa Tanzanite kwenye bei ya chini iliyopo hivi sasa ili iweze kupanda juu lakini pia tunataka kufanya tamasha la kupandisha Tanzanite juu ya mlima Kilimanjaro na hii itasaidia kupandisha thamani yake pia kufanya hivyo itawezesha kuendelea kuniambia dunia kuwa madini haya yanapatikana Tanzania peke yake,” Alisema Money.
Sambamba na hayo pia aliiomba serikali kutengeneza mfumo maalum kupitia tasisi za fedha ambayo itamfanya mchimbaji kupitia madini yake awena nguvu ya kuwa na fedha mfukoni na sio kulazimika kuuza kwa bei ambayo haiendani na uzalishaji kwa ajili ya kuweza kulipa fedha za madeni tuu huku wakikosa faida yoyote.
Kwa upande wake mchimbaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jumanne Athumani Alieleza kuwa wanakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa dhana za milipuko hivyo aliiomba serikali iweke ruzuku katika eneo hilo kwani bila mchimbaji hakuna madini .
Aliongeza kuwa wachimbaji wengi wamefilisika hivyo ni vyema wawasaidie kwani wao ndio wazalishaji ambapo pia waliomba serikali kuwapa uhuru wa kumiliki madini hayo kwani wanachimba, wanapata, wanayathaminisha lakini wanakosa uwezo wa kumiliki kutokana na sheria zilizopo.