Home BUSINESS SHIRIKA LA POSTA LAZIDI KUIMARIKA, MAPATO YAFIKIA BILIONI 33.7 MWAKA 2022/2023

SHIRIKA LA POSTA LAZIDI KUIMARIKA, MAPATO YAFIKIA BILIONI 33.7 MWAKA 2022/2023

Na. Beatrice Sanga-MAELEZO

Shirika la Posta limeendelea kutengeneza faida kutokana na shughuli mbalimbalui ambazo linazifanya pamoja na uwekezaji mzuri unaoendelea kufanywa na serikali ikiwemo kusafirsha bidhaa na huduma kwa haraka, ufanisi kwa njia za kidigitali, hivyo limejizatiti kuongeza utoaji wa gawio Serikalini.

Hayo yamesemwa August 14, 2023 Jijini Dar es Salaam na Macrice Mbodo Postamasta Mkuu wakati wa Mkutano wa Msajili wa Hazina, Shirika la Posta na Wahariri wa vyombo vya habari katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), ambapo amebainisha kuwa mwaka 2022/2023 ulikuwa ni mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mpango mkakati wa nane (8) wa kibiashara (2022/2023– 2025/2026) wa shirika hilo unaolenga kuifanya Posta ya Kidijitali kwa Biashara Endelevu katika uchumi wa kidijitali ifikapo mwaka 2025/2026.

“Mwaka 2022/2023 tumezalisha mapato ya jumla ya Tshs. 33.7 bilioni. Mapato haya ni ongezeko la asilimia 3.4 ikilinganishwa na mapato halisi yaliyozalishwa mwaka 2021/22 ambayo yalikuwa Tshs. 32.6. bilioni. Faida kabla ya kodi tuliyozalisha ni Tshs. 2.08 Bilioni sawa na ongezeko la asiilimia 16 ikilinganishwa na faida iliyozalishwa mwaka 2021/22 ambayo ilikuwa Tshs. 1.79 Bilioni.” Amesema Mbodo.

PostaMasta Mkuu huyo amesema kwa sasa Shirika limewekeza zaidi kwenye teknolojia kuliko kutumia njia ambazo zimekuwa zikitumika kwa muda mrefu, ili kurahisisha utoaji wa huduma kitaifa na kimataifa, ikiwemo kuwezesha maduka zaidi ya 1200 kuuza bidhaa mbalimbali ndani na nje ya nchi kupitia Duka la mtandaoni pamoja na kutangaza vivutio mbalimbali vya Tanzania kupitia stempu maalum za vivutio vikuu vitano vya Tanzania (Big five) ikiwa ni jitihada za kuunga mkono nia ya Serikali ya kuvutia watalii.

“Shirika limefanikiwa kuanzisha na kuzindua mfumo na programu tumizi ya Posta Kiganjani kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma za posta na biashara kupitia simu janja ambapo program hii inapatikana kupitia google play store na app store.” Amefafanua Mbondo.

Mbodo amesema Shirika hilo limeendelea kuimarisha usalama huduma zake ili kuhakikisha shughuli zake hazikwami kutokana na changamoto mbalimbali za kiusalama na kiulinzi na pia limekuwa likiwezesha huduma mbalimbali za kijamii, kiuchumi ikiwemo Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa kusafirisha na kusambaza vishikwambi vilivyotumika katika sensa hiyo, kusafirisha sampuli za kibaiolojia nchi nzima kutoka vituo mbalimbali vya afya na kwenda maabara za vipimo.

“Katika kipindi cha mwaka 2022/2023 Shirika limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa mali za wateja kwa kuongeza mitambo mitatu ya kisasa ya ukaguzi wa mizigo pamoja na kuongeza Kamera za kisasa (CCTV Camera) 200 kwenye ofisi mbalimbali za shirika Bara na Zanzibar. Kamera 200 zimenunuliwa na zimeshafungwa ofisi mbalimbali nchini.” Amesema Mbodo.

Aidha shirika la Posta kwa sasa limeendelea kutanua wigo wake wa utoaji huduma kwa kuimarisha na kusimamia Vituo vya huduma ya pamoja vya Dar es Salaam na Dodoma na kuanzisha vituo vitatu vipya Tanga, Mbeya na Mwanza ambapo kupitia vituo hivyo, kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 zaidi ya wananchi 100,000 wamehudumiwa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za Vitambulisho vya Taifa, (NIDA), RITA, Uhamiaji, TRA, BRELA, NHIF, NSSF, PSSF, Polisi.

Kwa upande wake Deodatus Balile Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) amesema kuwa Shirika hilo limepiga hatua kubwa kutokana na jitihada na uwekezaji unaofanywa na serikali, na ameiomba serikali ushirikiano huo kati ya serikali na vyombo vya habari usiishie kwenye mashirika ya umma pekee bali uende hadi ngazi ya Wizara ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa kati ya serikali na wananchi wake.

“Utaratibu huu uendelee si tu kwa mashirika ya umma bali hata wizara, zipo wizara ambazo kwakweli zinafanya mambo makubwa lakini Mawaziri wake wanateleza kuliko Kambale, lakini zipo Wizara zinafanya mambo ambayo hata hazijui zinafanya nini, nchi nyingi za ulimwengu wa tatu zinachelewa katika maendeleo siyo kwasababu hazina rasilimali, si kwasababu hazina watu wenye ujuzi, ni kwasababu ya mawasiliano, kwahiyo tujenge Utamaduni wa mawasiliano, tujenge utamaduni wa kuzungumza.” Amesema Balile

Previous articleFISI MWENYE KICHAA CHA MBWA ALIVYOJERUHI MKAZI NGORONGORO ,WAIOMBA SERIKALI KUWAHAMISHA HARAKA
Next articleIJUE SHERIA: HILI NDILO KOSA LA UHAINI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here