Home LOCAL WAZIRI DKT. GWAJIMA AITAKA DIASPORA URUSI KUCHANGAMKIA FURSA URUSI

WAZIRI DKT. GWAJIMA AITAKA DIASPORA URUSI KUCHANGAMKIA FURSA URUSI

Na.WAMJW.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Watanzania wanaoishi na kusoma nchini Urusi kutumia fursa zilizopo Tanzania katika kuwekeza na kuwasaidia Watanzania.

Dkt. Gwajima ameyasema hayo jijini Saint Petersburg nchini hapa alipokutana ma kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi na wanaosoma katika Vyuo mbalimbali.

Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa Tanzania ina fursa nyingi za kuwekeza katika Sekta mbalimbali katika kusaidia jamii ikiwemo Sekta ya Afya, Utalii na Madini ambazo zinaweza kuchangia katika Maendeleo ya Taifa.
Ameongeza kuwa kuishi au kusoma nje ya Tanzania hakufungi milango kuwekeza nyumbani na kuleta mabadiliko katika Taifa ulilotoka ila ndio linaongeza fursa na nafasi ya kuleta mabadiliko katika jamii kutokana na mambo mapya ya kujifunza kutoka Mataifa mengine.

“Niwaambie ndugu zangu nyumbani kumenoga wekezeni nyumbani haijalishi wewe unaishi huku au wewe ni mwanafunzi mnaweza mkajiunga pamoja na kuanzisha umoja wenu mkatafuta wafadhili mkiwa Urusi na mkawasaidia Watanzania wenzenu”  alisema Waziri Dkt. Gwajima.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania ipo pamoja na Watanzania wanaoishi na kusoma nje ya Tanzania kwani azma ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira rafiki katika kuhakikisha wanapata fursa za kuchangia katika maendeleo ya Taifa huko huko walipo ikiwemo kuwekeza katika Sekta mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Urusi Dkt.Switbert Mkama amemuhakikishia Waziri Dkt.Gwajima kushirikiana na Watanzania wanaoishi na kusoma nchini humo kuweza kupata fursa zilizopo Tanzania katika kuwekeza na kusaidia jamii katika Sekta mbalimbali.

“Mhe. Waziri tutawashika mkono hawa wenzetu huku na kuwapa taarifa za fursa zilizopo nyumbani ili waweze kutoa mchango wao katika maendeleo ya Taifa letu hata wakiwa nje ya Tanzania” alisema Mhe. Mkama.

Naye,Mkurugenzi wa Idara ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Msajili wa NGOs nchini Vickness Mayao amesema inawezekana kwa Watanzania wanaoishi na kusoma nje kuweza kujipanga na kufungua NGO nchini kwani taratibu zinaruhusu kuanzishwa kwa NGOs za Kimataifa nchini na kuwataka kuchangamkia fursa hiyo katika kuhakikisha wanatumika fursa walinazopata kuwa nje ya Tanzania kusaidia jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Watanzania wanaoishi na kusoma nchini Urusi Lucas Muchunguzi ameishukuru Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha Watanzania kupata fursa za kusoma nje ya nchi na wameaahidi kutumia uzoefu na elimu watakayoipata kusaidia kuleta mabadiliko na kichangi katika maendeleo ya Taifa.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here