Na:Mwandishi wetu
Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imesema kuwa itahakikisha miradi mbalimbali ya ujenzi wa majengo na nyumba za makazi na Biashara ambayo ipo katika hatua za utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2023,ikiwemo miradi ya Mkoa wa Mwanza, Arusha na Dar-es-Salaam inatekezwa .
Hayo yamesemwa Julai 11,2023, kwenye maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Juliaus Nyerere Jijini dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro wakati walipozungumza na waandishi wa habari alipokuwa kwenye Banda lao katika maonesho hayo.
Amesema, kupitia Wakala wa Majengo nchini (TBA) miradi hiyo inakamilika kwa wakati na hivyo kupunguza changamoto za ukosefu wa makazi hususani kwa watumishi wa umma, na wafanyabiashara.
Amesema Wanatarajia kuwa na ujenzi mkubwa wa nyumba Mkoani Arusha katika eneo la kaloleni, na kwamba, watatumia fedha za ruzuku kwa bajeti iliyopitishwa, pamoja na fedha za makusanyo ya ndani kwa maana ya mapato yatokanayo na nyumba walizopangisha.
Aidha amezungumzia ujenzi wa nyumba za makazi katika wilaya ya Temeke na kwamba mradi huo unakwenda vizur.
“Tunategemea kule kujenga Block 7, na kila Block litakuwa 144, tumeanza na Block 1 na tunaendelea, kwahiyo fedha kadri zitakavyokuwa zinapatikana tutaendelea na mradi huo.
“Tuna miradi mingi ambayo sasa hivi iko katika hatua za utekelezaji, na kama mnavyofahamu wakala wa majengo Tanzania ni moja ya taasisi zilizoko chini ya wizara ya ujenzi na uchukuzi, kwa hiyo tuna miradi mingi ambayo tutaanza kuitekeleza mara tu fedha zitakapoanza kutoka kutokana na Bajeti iliyopitishwa.
Amesema kuwa kutokana na makusanyo ya kodi mbalimbali katika miradi iliyopo chini ya wakala pamoja na ruzuku kutoka wizarani, watahakikisha ujenzi na umaliziaji wa miradi hiyo unakamilika, na kwamba mwakani katika maonesho ya sabasaba watakuwa na miradi mingi ambayo watakwenda kuonesha kupitia maonesho hayo.
Akielezea kuhusu mradi wa Magomeni amesema hadi sasa tayari kuna Block 1 la familia 12 ambalo limeshakamilika na watu wameanza kuingia, na Block la pili wanategemea kwamba itakapofika mwezi Disemba litakuwa limekamilika, pia wanategemea kutekeleza mradi wa Ghana, Jijini Mwanza ambapo wameanza ujenzi kwa kutumia vyanzo vyao vya ndani, lakini wanategemea kupata fedha za ruzuku kwa ajili ya mradi huo ambao utakuwa na maduka ya Biashara.
“Na katika kutekeleza agizo la Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kushirikisha Sekta Binafsi, kwa sasa wakala inajiandaa kuanzisha sera ya ubia ili kukaribisha Sekta Binafsi kuwekeza kwa njia ya ubia ikiwa ni jitihada za kuongeza ufanisi na uharaka katika upatikanaji wa mitaji, ujenzi wa miradi, kusimamia pamoja na kuongeza mapato kutokana na kuongezeka kwa shughuli za ujenzi,”amesema Kandoro.