Daktari Bingwa wa Mifupa na Majeruhi kutoka hospitali ya kanda-Kamanga Dkt. Fikiri Martin ametoa rai kwa waendesha vyombo vya moto kuweka kipaumbele cha afya zao kwani watakapopata ajali madhara yatabaki maisha yao yote.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani Dkt. Adam Gembe wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Pwani-Tumbi amewasisitiza wagonjwa wa Moyo,Kisukari kuzingatia matumizi sahihi ya dawa kulingana na maelekezo ya wataalam wa afya.
Mtaalamu wa afya katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora-Kitete akifanya uchunguzi kwa wagonjwa waliofika kupata matibabu ya kibingwa.
Mmoja wa wagonjwa waliopatiwa matibabu ya kibingwa akifurahia huduma alizopata na kuishukuru Serikali kwa maboresho katika hospitali nchini na hivyo kuwarahisishia huduma za afya wananchi.
Bw. Yusuph Kaba mkazi wa Tabora mjini akiongea na Mratibu wa huduma za rufaa ya Mkoa-Kitete Dkt. Nassib Msuya (mwenye koti jeupe) na kuwashukuru watoa huduma kwa upasuaji alofanyiwa na kuipongeza Serikali kwa maboresho waliyoyafanya hospitalini hapo.
Na: Catherine Sungura, Tabora
Wananchi pamoja na madereva wanaoendesha vyombo vya moto nchini wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari wanapokua wanatumia barabara kwa kufuata sheria za barabarani kuepusha ajali kwa wao wenyewe au watumiaji wa barabara ili kupunguza ajali na kuepushia Serikali kutumia gharama kubwa za kuwahudumia wagonjwa wanaotokana na ajali za hizo.
Rai hiyo imetolewa leo na Dakatari Bingwa wa Mifupa na Majeruhi kutoka hospitali ya Rufaa ya Kanda- Kamanga ya jijini Mwanza Dkt. Fikiri Martin wakati wa kambi ya utoaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wa mkoa wa Tabora inayofanyika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora-Kitete.
âNiwahimize wananchi wachukue tahadhari wanapotumia barabara kwa kufuata alama, sheria za barabarani na kwa wale wanaotumia vyombo vya moto kuwa na leseni na kuzihuisha leseni zao pia kuendesha vyombo hivyo wakiwa wanajihami ili kuepusha ajali kwa wao wenyewe au kwa watumiaji wengine wa barabaraâ.
Ameongeza kuwa ni vyema kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto kujenga mazoea ya kufunga mikanda na kwa madereva kuendesha magari kwa mwendo unaoendana na hali ya barabara.
Kwa upande wa madereva wa bodaboda Dkt. Martin amesema ni vyema waendelee kuvaa kofia ngumu na kuzingatia suala zima la mwendo pamoja na kuwajali abiria wao na wanaowapita barabarani.
âBoda boda ni ajira kubwa na tutaendelea kuwatumia hivyo ni vyema wakawa makini, wakaweka kipaumbele cha afya zao mbele kwani endapo atapata ajali na kuumia mguu au vinginevyo unakua na asilimia hamsini ukapona kabisa au ukatibiwa na kubaki na madhara maisha yako yote, kimsingi ni kuendesha kwa kufuata sheria za barabarani na kuweka maisha yako salama.
Kuhusu kambi hiyo ya utoaji wa huduma za kibingwa Dkt. Martin amewashukuru wananchi ambao wamejitokeza kupata huduma za kibingwa na zaidi ya wagonjwa wa mifupa mia mbili na hamsini wameonwa katika idara hiyo na baadhi ya wagonjwa waliopata ajali hivi karibuni wamefanyiwa upasuaji wa kuwekewa vyuma kwa ajili ya kuunga mifupa ipate muelekeo wake wa zamani.
Naye, mmoja wa wazazi waliopatiwa huduma za kibingwa idara ya mifupa katika kambi hiyo Bi. Helena Salumu anayeishi kata ya Kiloleni ameishukuru Serikali kwa kuwafikishia huduma hizo katika hospitali ya Kitete na kutoa ushauri kwa wazazi wengine kutokukata tamaa kwani huduma zipo na hivyo kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya kutolea huduma pale wanapoona matatizo na kuongeza kuwa mwanaye huyo mwenye umri wa miaka minne aliyapata matege hayo akiwa ameanza kutembea na kwamba motto wakealipokuwa akisimama.
-Mwisho-