Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Kampuni Tanzu ya Al Faisal (Al Faisal Holding ) Sheikh Faisal Bin Qassim Al Thani mara baada ya Mazungumzo yao yaliofanyika katika Mji wa Doha nchini Qatar leo tarehe 08 Machi 2023. (wengine ni Balozi wa Tanzania nchini Qatar Dkt. Mahadhi Juma Maalim, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Mbarouk).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 08 Machi 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni Tanzu ya Al Faisal (Al Faisal Holding ) Sheikh Faisal Bin Qassim Al Thani Mazungumzo yaliofanyika katika Mji wa Doha nchini Qatar.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais amemkaribisha mwekezaji huyo nchini Tanzania kuwekeza katika fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo ikiwemo katika miundombinu ya utalii kama vile Hoteli.
Pia Makamu wa Rais amesema Tanzania inayo fursa katika uwekezaji wa viwanda vya dawa , kilimo pamoja na madini.
Kutokana na serikali kuhamishia shughuli zake katika makao makuu ya nchi mkoa wa Dodoma, Makamu wa Rais amesema mkoa huo unayo fursa ya kuwekeza katika ujenzi wa nyumba za makazi, hospitali pamoja na hoteli.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kampuni Tanzu ya Al Faisal (Al Faisal Holding) Sheikh Faisal Bin Qassim Al Thani ameahidi kufanya ziara nchini Tanzania pamoja na ujumbe wake ili kushiriki majadiliano ya pamoja katika kuangazia maeneo muhimu ya uwekezaji ikiwemo elimu, afya na uongezaji thamani ya mazao ya kilimo.
Ameongeza kwamba Tanzania imejaaliwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji na kuahidi kuendelea kuwaalika wawekezaji wengine kutoka katika baraza la ushirikiano la ghuba (Gulf Cooperation Council) linalojumuisha nchi ya Qatar na nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu.
Sheikh Faisal Bin Qassim Al Thani ni mwenyekiti wa kampuni tanzu ya Al Faisal ilioanzishwa mwaka 1964 inajishughulisha na biashara mbalimbali ikiwemo umiliki wa hoteli kubwa zaidi 20 duniani kote, makumbusho ya kiutamaduni nchini Qatar, utengenezaji na usambaji dawa pamoja na uwekezaji katika ujenzi wa nyumba za makazi na biashara.