Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza katika mjadala uliobeba ajenda ya Uwekezaji kwa Watu Wote Pasipo Ubaguzi ulioshirikisha Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoshiriki Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea za Kipato cha Chini unaofanyika Doha Nchini Qatar.(Kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Saada Mkuya pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mbarouk N. Mbarouk nje ya Ukumbi wa Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea za Kipato cha Chini unaofanyika Doha Nchini Qatar.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameshiriki katika mjadala uliobeba ajenda ya Uwekezaji kwa Watu Wote Pasipo Ubaguzi ulioshirikisha Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoshiriki Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea za Kipato cha Chini unaofanyika Doha Nchini Qatar.
Akichangia katika mjadala huo, Makamu wa Rais amesema katika kuwekeza kwa watu Tanzania imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuboresha sekta ya elimu kwa kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kuboresha miundombinu ya shule pamoja na ujenzi wa shule za wanawake maalum kwa masomo ya sayansi kila mkoa wa Tanzania.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba ili kuendana na wakati wa sasa, Tanzania inafanya mabadiliko ya mitaala ya kufundishia pamoja na kujikita katika elimu ya tehama kwa kutoa vifaa vya kidijitali kwa walimu ili waweze kufanikisha lengo hilo. Pia amesema ili kuhakikisha elimu inakua jumuishi bila ubaguzi, Tanzania imefanikiwa katika kuwarudisha masomoni wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo za kupata ujauzito.
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa jumuiya za kimataifa kuendelea kuunga mkono mataifa yanayoendelea kutokana na uwepo wa changamoto katika uwekezaji kwa watu ikiwemo kukosekana fedha za kutosha katika kuboresha na kuongeza vyuo vya ufundi, upungufu wa vifaa vya kujifunzia hususani kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na ufinyu wa miundombinu ya kujifunzia kutokana na ongezeko la watu.
Makamu wa Rais yupo nchini Qatar kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea za Kipato cha Chini.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Machi 6, 2023
Doha – Qatar