Mkuu wa wilaya ya Makete Juma Sweda akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maji katika wilaya hiyo ambapo amewataka wakandarasi na wataalam wanaotekeleza miradi ya maji wilayani humo kuwa waadilifu na kutumia weledi kwenye utekelezaji wa miradi ya maji
Meneja wa Ruwasa mkoa wa Njombe Mhandisi Sadik Chakka akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ambapo alisema,katika kipindi cha miaka mitatu tangu Ruwasa ilipoanzishwa jumla ya vijiji 95 vimefikiwa na miradi ya maji yenye thamani ya Sh.bilioni 26.8.
Mbunge wa Jimbo la Makete Festo Sanga katikati akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Ruwasa wilayani Makete,wa pili kulia Afisa maendeleo ya jamii kutoka ofisi ya Ruwasa mkoa wa Njombe Seleman Mdaba
Na: Muhidin Amri, Njombe
WAKALA wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) mkoa wa Njombe,imetumia Sh.bilioni 26.8 kutekeleza miradi ya maji kwenye vijiji 95 ambayo imewanufaisha zaidi ya wakazi 158,000.
Hayo yamesemwa na meneja wa Ruwasa mkoa humo Mhandisi Sadick Chakka,wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ofisini kwake mjini Njombe,ambapo kabla ya hadi kufikia asilimia 75.9 mijini na vijijini huku upande wa vijijini huduma ya maji ikifikia asilimia 80.6.
Chakka alisema,miradi hiyo imetekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu tangu Ruwasa ilipoanzishwa mwaka 2019 hadi tarehe 30 Juni 2022 na fedha hizo zimeongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 17.6.
Alieleza kuwa, kabla ya Ruwasa haijaanzishwa huduma ya maji katika mkoa wa Njombe ilikuwa asilimia 63.4 na baada ya kukamilika kwa miradi hiyo huduma ya maji imefikia asilimia 80.6.
Aidha alisema,wameanza kutekeleza miradi mipya 21 kwa gharama ya Sh. bilioni 38.1 kwenye vijiji 43 vyenye wakazi 82,154 ambao watapata maji kwenye maeneo ambayo kwa sasa hakuna huduma hiyo.
Chakka alisema,kuna miradi mingine 21 imeanzishwa na baadhi iko hatua ya manunuzi ambayo itatekelezwa katika vijiji 48 na itagharimu shilingi bilioni 40 na sehemu kubwa ya miradi hiyo itakamilika kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mkuu wa wilaya ya MaketeJuma Sweda,ameishukuru wizara ya maji kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kusimamia na kutekeleza miradi ya maji ambayo imeanza na inakwenda kumaliza kabisa kero ya maji kwa wananchi wa vijijini.
Alieleza kuwa,kabla ya kuanzishwa kwa Ruwasa mtandao wa maji katika wilaya hiyo ulikuwa urefu wa km 483,lakini katika awamu ya sita mtandao umeongezeka hadi km 539.1 sawa na asilimia 56.1.
Alisema,mafanikio hayo yanatokana na serikali ya awamu ya sita kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi ya maji ambapo katika wilaya hiyo vijiji 87 kati ya 93 vimefikiwa na mtandao wa maji ya bomba,na watu 87,243 sawa na asilimia 90.1 wanapata huduma ya maji katika maeneo yao.
Sweda,amewataka wakandarasi na wataalam wa Ruwasa kutekeleza miradi ya maji kwa weledi,uadilifu na kuepuka udanganyifu ikiwamo kuongeza gharama za fedha,ili miradi inayotekelezwa iweze kuleta tija na kuwaondolea wananchi kero ya huduma ya maji safi na salama.
“Ni lazima tuhakikishe wakandarasi wanaopewa kazi ya ujenzi wa miradi hii na wataalam wetu wa Ruwasa wanazingatia suala la ubora,serikali inatoa fedha nyingi kwa lengo la kusogeza na kuboresha huduma ya maji ili kuharakisha maendeleo ya wananchi wetu” alisema.
Mkuu wa wilaya,amewapongeza wananchi wa wilaya ya Makete kwa kazi kubwa ya upandaji miti na kuiwezesha wilaya hiyo kuwa na vyanzo vingi vya maji, hata hivyo amewaasa kuvilinda ili miradi inayojengwa iweze,kudumu kwa muda mrefu.
Mbunge wa Jimbo la Makete Festo Sanga,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kutoa zaidi ya shilingi bilioni 7 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji ambayo itakapo kamilika itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa jimbo hilo.
Sanga alitaja baadhi ya miradi inayotekelezwa na fedha zake ni Usalimwani-Mfumbi (ml 900) Ujuni(ml 800) Sapilano- Makete(zaidi ya bilioni 3)Utweve(ml 300)Tandala (milioni 700)
na miradi ya Madiani-Lamagi na Upelele ambayo inakwenda kutekelezwa siku chache zijazo.
Alisema,wakati anaingia madarakani mwaka 2020 upatikaji wa maji katika jimbo la Makete ulikuwa asilimia 80,lakini sasa imefikia asilimia 91,na kuipongeza serikali na wataalam wa Ruwasa kwa kazi nzuri inayofanya katika kutekeleza miradi ya maji.
Akitoa taarifa ya upatikanaji wa maji meneja wa Ruwasa wilaya ya Makete Innocent Lyamuya alieleza kuwa,huduma ya maji katika wilaya hiyo yenye wakazi wapatao 112,00 ni asilimia 90.1,kati ya hao 96,500 wanaishi vijijini ambako Ruwasa wanatoa huduma hiyo.
Lyamuya alisema,kama wilaya ya wamejiwekea malengo ya kufikisha asilimia 93 ifikapo mwaka 2023 na asilimia 98 mwaka 2025, baada ya kukamilisha ukarabati wa baadhi ya miradi maji ya zamani ya Bulongwa-Magoma unaohudumia vijiji 14 na mradi wa kata ya Mang’oto unaohudumia vijiji vitano.
MWISHO.