Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ametoa wito kwa Wakulima kutumia fursa ya kuongeza uzalishaji wa malighafi.
Mhe. Kigahe Ameyasema hayo leo Tarehe 22 Novemba, 2022 aliposhiriki hafla ya upanuzi wa kiwanda cha kutengeneza Vinywaji vikali cha Serengeti Breweries Limited (SBL) kilichopo Mkoani Kilimanjaro.
Mhe. Kigahe ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anatambua kwa dhati juhudi kubwa zinazofanywa na Wawekezaji Nchini hasa katika kukuza uchumi na kufanya maisha ya wananchi wetu kuzidi kuboreka hivyo kutokana na kiwanda kuongeza mstari wa uzalishaji ni fursa kwa Wakulima kuongeza uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya kulisha kiwanda hiki.
Akizungumza kwa niaba ya Kampuni Bw. Mark Ocitti, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kiwanda cha Serengeti Breweries amesema Kampuni imewekeza kiasi cha Shilingi bilioni 185 katika kupanua shughuli za uzalishaji ambapo italeta fursa mpya za ajira, kuongeza mapato ya serikali na kuwanufaisha wadau wote wa Biashara hii.
Aidha, Bw. Ocitti ameongeza kuwa Nchi ya Tanzania ina hali ya hewa nzuri kwa Kilimo, idadi kubwa ya watu na hivyo kuvutia Uwekezaji katika Viwanda na Serikali ya awamu ya Sita imeboresha Mazingira ya Biashara Nchini kwa Wawekezaji wakubwa na Wadogo na changamoto zilizokuwa zinajitokeza zimekuwa zinasghughulikiwa kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mahusiano Bw. John Wanyancha amesema Kiwanda cha Serengeti Breweries tawi la Moshi asilimia sabini (70) ya malighafi inayotumika kiwandani hapo inatoka kwa wakulima wa ndani ya Nchi, na kiwanda kimeongeza matanki kumi (10 ) ya kuchachulia pombe, mstari mpya wa kupakia na sehemu ya uzalishaji wa pombe kali aina ya Sminorff Ice nyekundu na Nyeusi.