
Mwandishi Wetu
Ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, pamoja na Naibu wake Kaspar Mmuya, katika Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Januari 5, 2026, imekuwa tukio lenye uzito mkubwa katika mwelekeo wa sekta ya makazi nchini.
Ziara hiyo, ambayo pia ilikuwa ya kwanza kwa Waziri Akwilapo kujitambulisha rasmi katika shirika lililo chini ya wizara yake tangu ateuliwe, imebeba ujumbe mzito wa sera, uongozi na matumaini mapya kwa Watanzania wengi wanaokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa makazi bora na yenye gharama nafuu.

Kwa miaka 63 tangu kuanzishwa kwake, NHC imekuwa taasisi ya kimkakati katika utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, salama na yenye hadhi.
Hivyo basi, ujio wa Waziri na Naibu wake katika makao makuu ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam uliashiria dhamira ya dhati ya Serikali kuimarisha nafasi ya NHC kama chombo kikuu cha kutafsiri sera za makazi kuwa uhalisia unaogusa maisha ya wananchi.

Katika hotuba yake kwa menejimenti na watumishi wa NHC, Dk. Akwilapo alitoa maelekezo ya wazi na yenye mwelekeo wa muda mrefu, akisisitiza umuhimu wa utafiti wa kina katika kubuni na kutekeleza miradi ya makazi.
Alielekeza Shirika kufanya tafiti zitakazowezesha ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu, hususan kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kawaida. Kwa msisitizo, Waziri alieleza kuwa ‘unafu’ wa gharama lazima ueleweke kwa kuzingatia makundi tofauti ya Watanzania, hali zao za kiuchumi na mahitaji yao halisi.
Maelekezo hayo yameenda sambamba na wito wa kutumia teknolojia za kisasa na bunifu katika sekta ya ujenzi. Kwa mujibu wa Waziri, kupitia tafiti za kisayansi na ubunifu, NHC itaweza kupunguza gharama za ujenzi bila kuathiri ubora, huku ikizingatia mazingira, hali ya hewa, upatikanaji wa vifaa vya ujenzi na mitindo ya maisha ya jamii mbalimbali. Alibainisha kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za NHC katika utafiti na maendeleo (R&D), ikiwemo ushirikiano na taasisi za elimu ya juu, wataalamu wa ujenzi na sekta binafsi.


Zaidi ya hilo, Dk. Akwilapo aliitaka NHC kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi yake na kuepuka ucheleweshaji unaoongeza gharama.
Aliagiza pia Shirika kuimarisha ukusanyaji wa madeni ya wateja wake ili kuongeza mtaji wa ndani na uwezo wa kufikia malengo yake, akieleza matarajio yake kuwa ifikapo mwaka 2030, NHC itakuwa imechangia kikamilifu utekelezaji wa malengo ya Wizara na Serikali kwa mujibu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika ujumbe uliogusa moja kwa moja maisha ya wananchi, Waziri alieleza kuwa NHC ina uwezo wa kuwaondolea Watanzania mzigo wa ujenzi binafsi unaoambatana na changamoto za mafundi wasio waaminifu, gharama zisizotabirika na usimamizi mgumu wa miradi. kwa kujenga nyumba bora kwa gharama nafuu, NHC itasaidia kupunguza “msongo wa mawazo” unaowakabili wananchi wengi wanaojaribu kujenga makazi yao wenyewe.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Kaspar Mmuya alitoa wito wa kipekee na wa kuhamasisha kwa watumishi wa NHC. Aliwataka kuwa mfano bora wa kuishi katika makazi bora kwa kujenga au kumiliki nyumba zao binafsi, ili kuonesha kwa vitendo mafanikio ya sera na mikakati wanayoisimamia kitaaluma. Kwa msisitizo,
Mmuya alisisitiza kuwa watumishi wa NHC wanapaswa kuishi kwa hadhi inayolingana na dhamana yao, nidhamu na ufanisi, badala ya kuwa watazamaji wa mafanikio wanayoyahubiri.

Akizungumza mbele ya Waziri, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alimhakikishia Serikali kuwa Shirika litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa kuzingatia sera na miongozo yote ya Serikali.
Alieleza kuwa NHC inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya makazi na biashara nchini, na kubainisha kuwa mwaka 2026 Shirika lilipata tuzo tatu tofauti kutokana na utendaji bora, ikiwemo ulipaji wa gawio kwa Serikali.
Kwa mujibu wake, NHC imejipanga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ili kutimiza wajibu wake katika kufanikisha ajenda ya makazi bora, salama na nafuu kwa Watanzania.

Kwa ujumla, ziara ya Waziri Akwilapo na Naibu wake NHC imeacha taswira chanya ya ushirikiano imara kati ya Serikali na Shirika hilo.
Ni ziara iliyoweka mwelekeo mpya unaosisitiza utafiti, ubunifu, uwajibikaji na kasi ya utekelezaji, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea Tanzania yenye makazi bora, miji iliyopangwa na maisha yenye heshima kwa wananchi wote.





