Home BUSINESS DIRA YA KUBORESHA MAKAZI BORA KWA WANANCHI YA NHC YATUA KWA KAMATI...

DIRA YA KUBORESHA MAKAZI BORA KWA WANANCHI YA NHC YATUA KWA KAMATI YA BUNGE

– Utafiti na nyumba nafuu zatajwa suluhisho la baadaye

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

– Kamati ya Bunge yataka utafiti kwa vifaa, teknolojia za kisasa kupunguza gharama za ujenzi

– Enzi za Mwalimu Nyerere hadi Dira ya 2050, NHC yathibitisha uwezo wa taasisi za umma kujitegemea na kuleta tija.

Mwandishi Wetu.

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limebainisha mpango na mkakati wake wa kuboresha upatikanaji wa makazi bora yenye gharama nafuu nchini ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii,kwa kutolea ufafanuzi namna Shirika hilo litakavyojikita katika kutumia teknolojia za kisasa za ujenzi, utafiti wa kina wa vifaa mbadala pamoja na uendeshaji wa miradi kwa ufanisi wa kibiashara, unaolinda dhamira ya kijamii.

 

Akitoa wasilisho mbele ya Kamati hiyo ya Bunge, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, amebainisha hatua hizo zikiwemo za muda mrefu, kati na muda mfupi, kwenye  taarifa ya Shirika hilo Januari 15, 2026 Jijini Dodoma, akieleza kuwa NHC imejipanga kikamilifu kuendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye, kufuatana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Baada ya kupokea na kujadili taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mzava, amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kazi kubwa na yenye matokeo chanya, hususan katika eneo la ujenzi wa nyumba, usimamizi wa mali za umma na kuimarisha uwezo wake wa kifedha.

Mzava amesema Kamati imeridhishwa na mwenendo wa Shirika, lakini ikaelekeza kufanyika kwa utafiti wa kina zaidi kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa na vifaa mbadala vya ujenzi vitakavyosaidia kushusha gharama za ujenzi wa nyumba, hususan kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kati.

“Mahitaji ya makazi yanaongezeka kila siku. Suluhisho si kujenga nyumba nyingi pekee, bali kujenga kwa gharama zinazomudu wananchi. Tunaitaka NHC kushirikiana na taasisi za utafiti na wadau wa teknolojia kubaini njia mbadala zitakazopunguza gharama bila kuathiri ubora,” amesema Mzava.

Ameongeza kuwa Kamati iko tayari kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na NHC katika kuboresha sera, mifumo na mazingira ya kisheria yatakayowezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema Serikali inaunga mkono kikamilifu mwelekeo wa NHC wa kuwekeza katika teknolojia za kisasa za ujenzi na utafiti wa vifaa mbadala, akisisitiza kuwa hiyo ni sehemu ya ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata makazi bora kwa gharama nafuu.

Waziri huyo amesema Wizara itaendelea kushirikiana na NHC katika kuboresha sera na kanuni zitakazohamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba na kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi.

“Serikali inaiona NHC kuwa ni mshirika muhimu katika utekelezaji wa sera ya makazi. Mageuzi ya teknolojia, ubunifu na usimamizi thabiti ndiyo nguzo za kufikia lengo la nyumba bora kwa wote,” amesema Waziri huyo.

Awali, katika taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, ameeleza kuwa Shirika hilo lilianzishwa mwaka 1962 kupitia Sheria ya Bunge Na. 45, likiwa miongoni mwa taasisi za kwanza kabisa kuanzishwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, mwaka mmoja baada ya Uhuru wa Tanganyika.

Kwa mujibu wa Hamad, lengo la awali la NHC lilikuwa ni kuwapatia wananchi makazi bora na salama, sambamba na kusimamia na kuendeleza mali za majengo ya Serikali na wamiliki wengine, ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa kodi na matengenezo ya majengo.

Amefafanua kuwa katika hatua za mwanzo, NHC liliwezeshwa kifedha kupitia ruzuku ya Serikali (asilimia 47), mikopo ya Benki ya Nyumba na Serikali ya Shirikisho ya Ujerumani Magharibi (asilimia 40) pamoja na mapato ya ndani (asilimia 13), hali iliyoweka msingi wa Shirika kujitegemea hatua kwa hatua.

Mageuzi ya kisheria na kuimarika kwa ufanisi

Hamad amesema mwaka 1990 NHC liliundwa upya kupitia Sheria ya Bunge Na. 2 kwa kuunganishwa na aliyekuwa Msajili wa Majumba (RoB), hatua iliyopanua majukumu, rasilimali na wigo wa kiutendaji wa Shirika.

“Marekebisho ya mwaka 2005 yalilenga kulifanya Shirika liwe na ufanisi zaidi katika mazingira ya ushindani wa kibiashara, bila kupoteza dhamira yake ya msingi ya kutoa huduma kwa umma,” amesema Hamad.

Majukumu ya NHC, mwelekeo wa kimkakati

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu huyo, NHC lina majukumu makuu mawili ya kisheria:

Kwanza, kujenga nyumba za makazi na majengo mengine kwa ajili ya kuuza au kupangisha, pamoja na kutekeleza miradi ya ujenzi kwa mujibu wa mipango iliyoidhinishwa na Serikali.

Pili, kuzalisha au kuwezesha uzalishaji wa vifaa vya ujenzi, kusimamia miliki zake na za wamiliki wengine, kufanya matengenezo na kukusanya kodi za pango.

Katika utekelezaji wa majukumu hayo, NHC limeanza kuelekeza nguvu katika utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa za ujenzi, jambo linaloendana na maelekezo ya Kamati ya Bunge.

Mafanikio ya kifedha: NHC yavuka malengo kwa asilimia 138

Taarifa ya kifedha iliyowasilishwa imeonesha kuwa NHC limeendelea kuimarika kiuchumi.
Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Shirika lilipanga kupata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 30.10, lakini kufikia Juni 30, 2025, lilikuwa limepata faida ya shilingi bilioni 58.86, sawa na asilimia 138 ya lengo lililorekebishwa.

Aidha, gawio kwa Serikali limeongezeka kutoka shilingi bilioni 1.2 mwaka 2024 hadi shilingi bilioni 6 mwaka 2025, ishara ya mchango chanya wa NHC katika mapato ya Taifa.

Hamad ameeleza kuwa thamani ya mali za NHC imeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 6.3, ikichangiwa na ongezeko la miradi ya ujenzi wa nyumba, majengo ya biashara na umiliki wa ardhi.

Nyumba za gharama nafuu na miradi ya kimkakati.

Katika eneo la makazi, Hamad ametaja utekelezaji wa Samia Housing Scheme, mpango wa ujenzi wa nyumba 5,000 za gharama ya kati na chini unaotekelezwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam na Dodoma, ukiwa na lengo la kuwahudumia Watanzania wa kipato cha chini na cha kati.

Mbali na hilo, NHC linaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa majengo ya wizara jijini Dodoma, hospitali, masoko, shule na majengo ya biashara, miradi ambayo imeongeza ajira, kuboresha mandhari ya miji na kuchangia mapato ya Serikali.

Ushirikiano na dira ya 2050.

Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imehimiza kuendelea kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, NHC na wadau wa sekta binafsi ili kuhakikisha mageuzi ya sekta ya makazi yanakuwa endelevu.

Kwa mwelekeo wa mwaka 2026 na kuendelea, NHC limeweka kipaumbele katika kukamilisha miradi iliyosimama, kuanzisha miradi mipya, kutafuta ardhi ya gharama nafuu na kuimarisha utafiti wa teknolojia za ujenzi, hatua zinazoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa ujumla, pongezi za Bunge kwa Shirika la Nyumba la Taifa si tu kutambua mafanikio yaliyofikiwa, bali ni wito wa kuongeza kasi ya mageuzi, ubunifu na usimamizi bora. Katika safari ya zaidi ya miongo sita, NHC limeendelea kuthibitisha kuwa taasisi za umma zinaweza kujitegemea, kuwa na tija na kuwa mhimili wa maendeleo ya Taifa, ambapo makazi bora yanakuwa haki inayofikika kwa Watanzania wengi zaidi, si ndoto ya wachache.