
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya Chama Cha Mapinduzi CCM kuelekea Mwaka 2030 ni kuiwezesha Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara kuweza kuzalisha ngano Tani Milioni moja kwa mwaka katika jitihada za kuifanya Tanzania kuweza kujitegemea katika uzalishaji wa zao hilo la biashara.
Dkt. Samia amebainisha hayo leo Ijumaa Oktoba 03, 2025 wakati akiomba kura kwa maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara Kwenye uwanja wa Hanang, akisisitiza kuwa katika jitihada za awali kuwezesha mpango huo ni pamoja na kuendelea kutoa ruzuku za pembejeo za kilimo na mbolea pamoja na kuchukua mashamba yasiyoendelezwa kutoka kwa wawekezaji wa baadhi ya mashamba.
“Haipendezi kwamba tuna mashamba ambayo yangeweza kuzalisha ngano lakini tunaagiza ngano nyingi kutoka nje huku mashamba yakiwa hayazalishi, kwahiyo tutayaangalia mashamba hayo ya Gidagamot, Murjanda na Sechet na tumeitaka mamlaka kuangalia jinsi tunavyoweza kuichukua.” Amesisitiza Dkt. Samia.
Katika hatua nyingine Dkt. Samia ameeleza kufahamu kuhusu shamba la Basotu Plantation na kusema kuwa serikali imeamua kuwa shamba hilo lisalie chini ya Msajili wa hazina na likisimamiwa na Halmashauri ya Hanang, akiagiza Halmashauri hiyo kuacha urasimu na kuepuka vishoka kwa kuweka bei ya ukodishaji wake hadharani ili wananchi wafahamu.





