Dar es Salaam
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limezindua rasmi mauzo ya nyumba katika miradi mikubwa ya kisasa jijini Dar es Salaam na mikoa ya Tanga na Tabora. Uzinduzi huo umefanyika Makao Makuu ya NHC, Kambarage House, ukiongozwa na Meneja Mauzo na Masoko, Deogratius Batakanwa, ambaye amesema hatua hii inalenga kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, ya kisasa na yenye thamani ya kudumu.
Katika Dar es Salaam, NHC imezindua Boulevard Residence yenye nyumba za chumba kimoja (37.7 sqm), vyumba viwili (103.5 sqm) na vyumba vitatu (124.2 sqm), pamoja na Samia Housing Kijichi Residence yenye nyumba za chumba kimoja (32.02 sqm), vyumba viwili (62.70 sqm) na vyumba vitatu (95.30 sqm).
Kwa mkoa wa Tanga, NHC inatangaza mauzo ya nyumba kwenye Mkwakwani Plaza zenye vyumba viwili (80 sqm) na vitatu (108 sqm), huku mkoani Tabora ikijenga Tabora Plaza yenye vyumba viwili (95 sqm) na vitatu (124 sqm).
Bei za nyumba hizi zimepangwa kwa kuzingatia mahitaji ya Watanzania wa kipato tofauti, na lengo kuu ni kutoa fursa kwa kila mmoja kumiliki nyumba bora. Wateja wanaweza kupata huduma kwa kupiga namba ya huduma 0736 114 433 au kuwasiliana moja kwa moja na maafisa mauzo walioteuliwa.
Batakanwa amesema NHC itaendelea kujenga taifa kwa kutoa makazi bora na kuwataka Watanzania kutumia fursa ya kipekee ya kumiliki nyumba katika maeneo yenye miundombinu bora na mazingira salama. Kupitia miradi hii, NHC imeonesha dhamira ya kuharakisha maendeleo ya makazi nchini na kuwapa wananchi fursa ya kuishi na kufanya biashara katika mazingira ya kisasa.