Home LOCAL NCHIMBI AAHIDI UAMINIFU NA UCHAPAKAZI KUTIMIZA NDOTO NA MAONO YA DKT. SAMIA

NCHIMBI AAHIDI UAMINIFU NA UCHAPAKAZI KUTIMIZA NDOTO NA MAONO YA DKT. SAMIA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea Mwenza wa nafasi ya Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amemuhakikishia Mgombea Urais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ikiwa watapewa ridhaa ya kuunda serikali atakuwa msaidizi mwema, mchapakazi na uaminifu wa juu ili ndoto zake na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2025/30 iweze kukamilika kikamilifu na kuwanufaisha wananchi wa Tanzania.

Amemshukuru Dkt. Samia pia kwa kumuamini kushika nafasi ya Balozi, Kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na nafasi ya sasa ya kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Mgombea mwenza, akisema amezunguka katika Mikoa 27 ya Tanzania akiinadi Ilani ya CCM na kueleza kuwa Watanzania wameridhika na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2025/30.

Balozi Nchimbi amebainisha hayo leo Jumanne Oktoba 28, 2025 kwenye Viwanja vya CCM Kirumba Mkoani Mwanza, wakati wa ufungaji wa Kampeni za Mgombea wa nafasi ya Urais wa Tanzania kwa Tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akimuhakikishia pia ushindi wa kishindo Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na hatua kubwa za maendeleo zilizopigwa katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.

“Watanzania wametutuma kwako tukueleze kwamba kesho watakupa kura ambazo hazijapata kutokea na hii ni matokeo ya uchapakazi wa hali ya juu ulioufanya ukitanguliza mbele mahitaji na matarajio ya watu wetu, ukizisimamia serikali zetu kutimiza wajibu wake, lakini vilevile ukiisimamia CCM katika kuzisimamia serikali zetu. Nataka nikuhakikishie, kw mambo tuliyoongea na wananchi na mambo waliyotuahidi, zawadi wanayokwenda kukupa kwa uhakika ni ushindi wa kishindo.” Amesema Balozi Nchimbi.

Nchimbi pia ameeleza kuwa wananchi kote alikopita wana matarajio na imani kubwa na Dkt. Samia, akimuomba kujua kuwa watanzania wengi wanaamini kuwa hatowaangusha katika kutimiza matarajio ya wananchi na kusisitiza kuwa baada ya miaka mitano ni matamanio yake kuwa simulizi za mafanikio ziwe kubwa zaidi katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.