Home Uncategorized DKT.SAMIA AANDIKA HISTORIA MPYA KWENYE KAMPENI ZAKE, MWANZA WAMSUBIRI KWA SHAUKU KUBWA

DKT.SAMIA AANDIKA HISTORIA MPYA KWENYE KAMPENI ZAKE, MWANZA WAMSUBIRI KWA SHAUKU KUBWA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan Wiki hii anatarajiwa kuendelea na Kampeni zake kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa, akianza na Mkoa wa Mwanza Oktoba 07, 2025 na baadaye kuzuru Mikoa ya Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara na Mkoa wa Kagera.

Wananchi wa Mwanza wameonesha shauku yao ya kutaka kumuona na kumsikiliza, wakati huu ambao miradi mingi yametekelezwa Mkoani humo, la karibuni zaidi likiwa ni uzinduzi rasmi wa daraja la JP Magufuli lenye kuunganisha upande wa Kigongo na Busisi pamoja na ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli kwenye Ziwa Viktoria, uwezeshaji wa shughuli za uvuvi.

Jana Jumapili Oktoba 05, 2025 wakati akitoa tathmini ya Kampeni hizo, Katibu wa Itikadi, uenezi na mafunzo wa CCM Ndg. Kenani Laban Kihongosi alieleza kuwa kufikia jana Dkt. Samia tayari amefanya mikutano 77 kwenye Mikoa 21 ya Bara na Visiwani, akiwafikia zaidi ya watu 14, 600, 000 waliofika moja kwa moja kwenye Mikutano yake ya Kampeni.

Aidha wananchi wengine zaidi ya Milioni 31, 500, 000 wamefuatilia kampeni hizo kupitia Vyombo vya habari na Mitandao ya kijamii, akiwashukuru wananchi kwa hamasa na kujitokeza kwao kwa wingi na kuwaalika kwenye Kampeni hizo kwenye awamu ya mwisho inayoanza Jumanne hiii huko Mkoani Mwanza.

Dkt. Samia katika kampeni zake ameahidi kuwa ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali atazalisha ajira Milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi kufikia mwaka 2030, akiahidi pia kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi ili kuwezesha wananchi hususani wa kipato cha chini kujenga nyumba bora na za kisasa na kwa gharama nafuu pamoja na kuandaa na kutekeleza mkakati wa kutumia teknolojia zinazoibukia ikiwemo akili unde ili kuimarisha ufanisi na tija katika uzalishaji na utoaji wa huduma.

Kwa upande wa sanaa, maonesho na michezo kama sehemu ya kutoa fursa za ajira, Dkt. Samia kupitia Ilani anayoinadi wameahidi kujenga studio za uzalishaji filamu zinazotumia teknolojia na vifaa vya kisasa, kujenga kituo kikubwa cha burudani (Arena) kwaajili ya maonesho ya kazi za sanaa pamoja na kuanzisha na kuendeleza shule za michezo (Sports Academy) kwa lengo la kuandaa wana michezo wa leo na baadae sambamba na kujenga viwanja vya kisasa vya michezo vyenye viwango vya Kimataifa ikiwemo FIFA na Olympic ikiwemo Kiwanja na Mji wa AFCON City huko Mkoani Arusha.