Home SPORTS DKT. SAMIA AAHIDI KUKUZA UTALII, KUENDELEZA MICHEZO ARUSHA

DKT. SAMIA AAHIDI KUKUZA UTALII, KUENDELEZA MICHEZO ARUSHA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha na kukuza utalii Mkoani Arusha kwa kuboresha na kuja na vivutio vingi zaidi pamoja na kukuza utalii wa michezo.

Dkt. Samia ameyasema hayo leo Alhamisi Oktoba 02, 2025 Jijini Arusha kwenye muendeleo wa Kampeni zake kwenye Viwanja vya Michezo vya Sheikh Amri Abeid, akieleza kwamba serikali yake imeboresha na kupanua uwanja wa ndege wa Arusha na kuanzia Januari 2026, Uwanja huo utaanza kufanya kazi usiku na mchana na hivyo kukuza biashara, utalii na kurahisisha shughuli za usafiri kwa Watanzania.

Katika Miaka mitano ijayo, Dkt. Samia ameahidi ujenzi wa Ukumbi mkubwa zaidi wa Kimataifa wa mikutano utakaokuwa na uwezo wa kuhudumia watu 6,000 kwa wakati mmoja, ukiwa pia na huduma nyinginezo ikiwemo hoteli pamoja na kujenga kituo cha urithi wa Kijiolojia Ngorongoro Lengai ili kunufaisha na kuvutia zaidi watalii, wanasayansi watakaopenda kujifunza masuala ya kihistoria, Ikolojia pamoja na sayansi.

Katika upande wa Utalii wa michezo, Dkt. Samia ameeleza kuwa ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali, amepanga kukuza utalii wa michezo Mkoani Arusha pamoja na kusimamia kikamilifu ujenzi wa uwanja wa michezo wa AFCON uliofikia asilimia 63 hivi sasa, akisema ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Julai mwakani ukienda sambamba na ujenzi wa Mji wa AFCON katika eneo la Bondeni City Jijini Arusha ili kuvutia zaidi wageni na watalii wanaofika kwenye Mkoa huo.