Na Mwandishi wetu, Kiteto
MKUU wa Wilaya ya Kiteto, Remidius Emmanuel amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotolewa na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) zikiwemo za kusambaza bidhaa mbalimbali kwenye mradi huo.
DC huyo wa kiteto ametoa rai hiyo jana wakati wa kongamano la kuchambua fursa za kiuchumi lililoandaliwa na EACOP kwa kushirikiana na kampuni ya ujenzi wa bomba hilo ya China Petroleum Pipeline Co. Ltd (CPP) likiwa na leno la kuwaimua kiuchumi.
“Tuna kila sababu ya kuushukuru mradi huu, kwani unajali utu na maendeleo ya wananchi, ndiyo maana leo hii tunaona wanatoa njia za namna bora ya kupata nafasi ya moja kwa moja ya kupata tenda na fursa mbalimbali ndani ya mradi huu” alisema Emmanuel.
Kwa upande wake Mratibu wa Mahusiano ya Jamii kutoka EACOP Lawrence Sigala alisema kuwa wanatekeleza sera yao ya kutoa fursa kwa wazawa wanaouzunguka mradi huo ili waone tija ya uwepo wa mradi huo na mchango wao kwa jamii inayowazunguka.
“Tunataka kufanya kazi na jamii na wafanyabiashara wa ndani kwa sababu ukuaji wao ni sehemu ya ukuaji wa mradi huu na ni fahari yetu”, alibainisha Bw Sigala.
Pamoja na hayo aliweka wazi kuwa wafanyabiashara na wajasiriamali wazingatie ubora wa bidhaa watakazokuwa wanape;leka kwenye mradi ili ziwe na soko zuri kwa sababu mara zote wateja hupenda bidhaa zenye ubora na zenye kukidhi mahitaji yao.
“Napenda kutoa wito kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa hapa Kiteto kuongeza ubunifu, kushirikiana na kudumisha taaluma ili kunufaika ipasavyo na mradi wa EACOP”, alisisitiza Bw. Sigala.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa wilaya ya Kiteto Bi. Mufandii Msaghaa aliwahimiza wafanyabiashara kuwa na mshikamano katika utendaji wao wa kazi, na kupeleka bidhaa zinazohitajika na wateja.
“Kupata elimu ya biashara kama hii katika maeneo mengine yakupasa kulipia fedha, lakini sisi tujivunie uwepo wa EACOP tumenufaika kwa elimu hii ya bure kabisa”, alisisitiza Bi. Msaghaa
Wanahisa wa EACOP ni TotalEnergies yenye asilimia (62), Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) yakimiliki asilimia 15 kila moja na kampuni ya mafuta ya Kichina (CNOOC) ikiwa na asilimia nane.
Bomba la EACOP lina urefu wa kilometa 1443, linaanzia Wilaya ya Hoima nchini Uganda na kuishia nchini Tanzania katika Mkoa wa Tanga. Bomba hilo limepita katika mikoa nane ya Tanzania bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.
MWISHO