
Aliyekuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Mchinga kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 kupitia Chama Cha CHAUMMA Bw. Yusuph Issa Tamba ametangaza kujiunga na Chama Cha Mapinduzi CCM akipokelewa na Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt. Asharose Migiro mbele ya Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama hicho Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Bw. Tamba amepokelewa kwenye Mkutano wa kampeni za Dkt. Samia leo Septemba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi Mjini, akieleza kuwa amerudi nyumbani na kuwaonya baadhi ya wanachama na Viongozi wa Chama chake cha zamani CHAUMMA ambao wamekuwa wakimtumia meseji za vitisho kwenye simu yake ya mkononi.
“Leo yamenishinda baada ya kuona ilani ya Chama Cha Mapinduzi nikahisi najidanganya na nadanganya wananchi wa Jimbo la Mchinga. Mhe. Rais mimi kama mwanao kwa heshima na ridhaa yangu mwenyewe siku ya leo ninaunga jitihada za CCM na ninaomba wananchi wote wa Mchinga na Tanzaniakwa ujumla tumuunge mkono Dkt. Samia na tumpe mitano tena.Natuma salamu ka Chama changu CHAUMMA, meseji zimeingia za vitisho waambie mtoto mdogo mimi sitishiki, nimeamua nimerudi nyumbani, wao wananitisha mimi huku nipo nyumbani sitishiki, mitano tena.” Amesisitiza Bw. Tamba.
Mbali ya Tamba, wengine waliojiunga na Chama Cha Mapinduzi CCM ni pamoja na Salum Baruan, Mbunge wa zamani kupitia CUF na Makamu mwenyekiti wa zamani wa Chadema Kanda ya Kusini kwasasa akiwa ni Mwenyekiti wa Jimbo la Lindi Mjini Chadema pamoja na Rehema Muhema, Mjumbe wa Baraza kuu la Uongozi Chama cha wananchi CUF pamoja na wanachama wengine wa Chadema na CUF.





