Home BUSINESS DKT. SAMIA TUTAIFANYA TANGA KUWA BOHARI YA MAFUTA NA GESI

DKT. SAMIA TUTAIFANYA TANGA KUWA BOHARI YA MAFUTA NA GESI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu Septemba 29, 2025 amesema ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, serikali yake itajenga soko kubwa la kisasa kwa Wafanyabiashara wadogo Jijini Tanga, soko litakalogharimu takribani Shilingi Bilioni moja na Milioni 900 likiwa na uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara wadogo takribani 1400.

Dkt. Samia ameyaeleza hayo leo Jumatatu wakati wa Mkutano wake wa Kampeni kwenye Viwanja vya Usagara Sekondari, akibainisha kuwa ujenzi wa soko hilo unafuatia jitihada nyingine zilizofanywa Mkoani Tanga na serikali ya awamu ya sita katika ujenzi wa jengo la Kitega uchumi lililojengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni nane na Milioni mia saba ili kujibu mahitaji ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga.

Ameahidi pia kuendelea kuwajengea uwezo Wavuvi wa Mkoa wa Tanga ili waendelee kufanya uvuvi wa kisasa kwa kuwapatia nyenzo na kujenga miundombinu wezeshi ikiwemo ahadi ya ujenzi wa soko la samaki la Kimataifa la Kipumbwe Jijini Tanga.

Katika jitihada za kuinua hali za Wavuvi wa Mkoa huo, serikali ya awamu ya sita pamoja na mambo mengine, ilitoa Boti 15 kwa wavuvi wa Wilaya ya Pangani ili kuwawezesha kutanua zaidi eneo la uvuvi baharini suala ambalo limeongeza idadi ya samaki wanaovuliwa pamoja na kipato cha Wavuvi na Pato la Mkoa wa Tanga kwa ujumla.