Home SPORTS NHC YAUPIGA MWINGI BONANZA LA MICHEZO NANE-NANE

NHC YAUPIGA MWINGI BONANZA LA MICHEZO NANE-NANE

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na: Mwandishi wetu, DSM

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeungana na Taasisi mbalimbali nchini kushiriki bonanza la michezo wa mpira wa miguu (Nanenane Stuff Foot Ball Tounerment) lililoandaliwa kwa ajili ya kuadhimisha Sikukuu ya Wakulima, kwa lengo la kuimarisha umoja na mshikamano, pamoja na kuimarisha afya za wafanyakazi.

Akizungumza wakati wa bonanza hilo lililofanyika leo Agosti 8, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Michezo kutoka NHC, Veronica Mtemi, amesema ushiriki wao katika bonanza hilo umeleta manufaa makubwa kwa kuimarisha ushirikiano baina ya wafanyakazi na taasisi nyingine pamoja na kuboresha afya za washiriki.

“Kwa kutambua umuhimu wa michezo kazini, NHC imeanzisha utaratibu wa kushiriki shughuli mbalimbali za michezo kila siku ya Ijumaa baada ya kazi, ikiwa ni pamoja na riadha,” amesema Bi. Mtemi.

Ameongeza kuwa: “Wafanyakazi wa NHC hushiriki michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu, netiboli, karata, bao, ‘pool table’ ambayo uongeza mshikamano na hari ya kufanya kazi kwa bidii.”

Kwa upande wake, Meneja wa timu ya NHC,Said Bungara, amesema kuwa bonanza hilo limekuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya timu yao kuelekea mashindano ya Shirikisho la Michezo kwa Taasisi za Umma (SHIMUTA), na kuongeza kuwa mashindano hayo yamehusisha timu 10 kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi.

“Tunaamini kuwa michezo si tu burudani bali ni sehemu ya kujenga afya, nidhamu na mshikamano kazini,” amesema Bungara.

Naye Nahodha wa Timu ya Mpira wa Miguu ya NHC, Simon Mhiliwa, amesema bonanza hilo limekuwa chachu ya kuimarisha timu yao na kuongeza morali kwa ajili ya mashindano yajayo, huku akitoa shukrani kwa uongozi wa shirika kwa kuwezesha ushiriki wao na kuonesha dhamira ya kuendeleza michezo kazini.

Akizungumza katika bonanza hilo, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika hilo, Domina Rwemanyira, amesema bonanza hilo limekuwa jukwaa la kukuza ushirikiano baina ya wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali, na kutoa mwito kwa wana michezo hao kuchangamkia fursa zinazotolewa na NHC kwa kumiliki Nyumba bora za Shirika hilo,

Mwisho.