_▪️Awataka wasanii wawekeze zaidi katika sanaa ili kuongeza wigo wa ajira_
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema sekta ya utamaduni na Sanaa ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wasanii na Taifa, kuongeza fursa za ajira, kurasimisha kazi za sekta sambamba na kuimarisha maadili ya jamii.
Waziri Mkuu ametoa wito kwa wasanii nchini waweke kipaumbele cha kuwekeza mapato yatokanayo na kazi zao katika shughuli za mnyororo wa thamani wa sanaa ili kuongeza wigo wa kuajiri vijana katika sekta hiyo na kuongeza pato la Taifa.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Mei 17, 2025) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Wadau wa Utamaduni na Sanaa uliofanyika kwenye Ukumbi wa Millenium Tower jijini Dar es Salaam. Amesema sekta hizo zimeajiri makundi yote jumuishi yakiwemo ya watu wenye ulemavu, vijana, wazee na watoto kwa jinsia na hali tofauti na watu wote.
Waziri Mkuu amesema zaidi ya hayo, sekta hiyo inakuza ujasiriamali na biashara ndogondogo na za kati. ”Sote tumewashuhudia wasanii wakianzisha biashara, kuzirasimisha na kuziweka katika mfumo unaotambuliwa na mabenki ili kuzitumia kama dhamana kwenye taasisi za kifedha ili kupata mitaji kwa shughuli mbalimbali.”
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wasanii wote nchini wajitahidi kutengeneza kazi bora zaidi na kurasimisha shughuli zao za sanaa katika mamlaka husika za binafsi na Serikali ili kila msanii awe rasmi na aweze kunufaika na fursa zilizopo.
Amesema Sekta za Utamaduni na Sanaa inatoa mchango mkubwa katika uchumi kote ulimwenguni, ambapo Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ya mwaka 2022, imebainisha kuwa sekta hizo zilichangia asilimia 3.1 ya Pato la Dunia (GDP), huku ikitoa asilimia 6.2 ya ajira sawa na ajira milioni 50 duniani kote.
Waziri Mkuu amesema kwa kutambua umuhimu wa sekta za utamaduni na sanaa, Serikali imefanya jitihada mahsusi za kuendeleza sekta hizo. Jitihada hizo ni pamoja na kuimarisha mifumo kisera na rasilimalifedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kisekta.
Pia, Waziri Mkuu amesema sambamba na kutunga sera, Serikali imetunga sheria na kanuni zilizoleta mageuzi ya shughuli za utamaduni na sanaa. ”Mifumo hiyo ya kisheria, imewezesha shughuli za utamaduni na sanaa kuondoka kwenye dhana ya kuwa burudani pekee na kuwa ajira rasmi zinazochangia kukuza pato kwa mtu binafsi na Taifa.
Amesema hatua hiyo kwa upande mwingine ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 Ibara ya 241 inayoielekeza serikali kuboresha tasnia ya sanaa nchini ili kuiendesha kibiashara na kuongeza upatikanaji wa fursa zaidi za ajira kwa makundi yote ya jamii.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi amesema Mkutano huo ni wa pili katika mfululizo wa mikutano ya wadau wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania inayolenga kuwakutanisha ili kubadilishana uzoefu, kujadili mafanikio na changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo.
Akizungumzia kuhusu mahitaji ya mikopo kwa wasanii amesema ni makubwa kuliko mtaji walionao na kwa upande mwingine wadau wanaomba kiasi cha juu cha mkopo kinachotolewa cha shilingi milioni 100 kiongezwe mara dufu ili kiendane na uhalisia wa uwekezaji kisekta.
“Tumetoa mikopo yenye masharti nafuu kwa zaidi ya miradi 580 ya wasanii, hii inaonesha kwamba Serikali imedhamiria katika kuiinua sekta ya Utamaduni na Sanaa kama kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Hadi sasa tumefanikisha marejesho kwa asilimia 96 hadi sasa, jambo ambalo linaonesha uwajibikaji wa wanufaika.”
Amesema wakati wizara inaendelea na jitihada za kutafuta vyanzo vingine endelevu vya fedha, wanamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za makusudi za kuhakikisha bajeti ya Mfuko wa Utamaduni inaongezeka kila mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 imefikia sh bilioni nne kutoka shilingi bilioni 1.6 mwaka 2023/2024.