Home Uncategorized DKT. NCHIMBI ATUMIA LUGHA LAINI SANA KUJIBU ‘NO REFORM NO ELECTION’ YA...

DKT. NCHIMBI ATUMIA LUGHA LAINI SANA KUJIBU ‘NO REFORM NO ELECTION’ YA CHADEMA

*Asema CCM inauwaunga mkono wakiamua kususia uchaguzi mkuu

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

*Asisitiza ni kosa kukilazimisha chama cha siasa kushiriki uchaguzi

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Emmanuel Nchimbi ameweka wazi hakuna sababu ya kuilazimisha CHADEMA kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwani vyovyote watakavyoamua iwe kushiriki au kutoshiriki ni sawa.

Amesema ni kosa kubwa kukilazimisha chama cha siasa kushiriki uchaguzi huku akibainisha hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kuzuia Uchaguzi Mkuu.

Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu Maalum wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF) unaofanyika Songea Mjini mkoani Ruvuma leo, Dk.Nchimbi ametumia nafasi hiyo kuzungumzia ya kauli mbiu ya ‘No Reforms No Election’ ya CHADEMA ambayo lengo lake ni kuzuia uchaguzi mkuu mwaka huu.

Akitumia sauti ya upole iliyokuwa ikipenya katika masikio ya kila mhariri aliyekuwepo katika mkutano huo, Dk.Nchimbi amesema nchi yetu inautaratibu wa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano.

“Tumekuwa tukifanya hivyo tangu mwaka 1961 ,kila baada ya miaka mitano Uchaguzi Mkuu. Ukifika mwaka wa uchaguzi mkuu hakuna raia yeyote anayeweza kuzuia uchaguzi

“Hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawezi, hata Makamu wa Rais hawezi, Waziri Mkuu hawezi kulitamkia Taifa kuzuia uchaguzi mkuu.

“Kwasababu hilo ni takwa la kikatiba ,ninataka niwahakikishie sio wahariri bali Watanzania wote kuwa uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais mwaka 2025 utafanyika.”

Dk.Nchimbi pia amesema pamoja na haki ya kuchagua na kuchaguliwa ni kosa kubwa kukilazimisha chama kingine cha siasa kuingia kwenye uchaguzi.

Amesisitiza ameanza kusikia taarifa za baahi ya wananchi na wengine wana CCM wakishinikiza CHADEMA iingie kwenye Uchaguzi Mkuu.

“Ni haki  yao kususia na uchaguzi huu sio wa mwisho, nataka niwape salamu zao CHADEMA yupo rafiki yangu pale Tundu Lissu watu wasiowaonee bure uchaguzi huu sio wa mwisho.

“Kuna uchaguzi mkuu mwingine mwaka 2025, 2030,2035,2040,2045, 2050 na kuendelea…wakikosa kufanya uchaguzi huu iko miaka mingine ya uchaguzi. Mtu yeyote asiwalazimishe ni haki yao kugomea.

“Kwa mujibu wa Katiba yetu hata chama kikiwa kimoja kinagombea wananchi watapiga kura ya ndio au hapana. Kuwasema sema CHADEMA sio sawa.

“Kwa hiyo namwambia rafiki yangu Tundu Lissu anahaki ya kuzuia chama chake kutogombea na tutawaunga mkono vyovyote watakavyoamua.

“Kugombea na kutogombea vyote ni sawa, ni haki yao. Hata hivyo kama watagomea wasisahau kura zao au sio… ndio jadi yetu kwani ukikosa haki ya kuchaguliwa usipoteze haki ya kuchagua.

“Angalau katika hizo haki mbili hakikisha unaipata mojawapo. Ukishindwa kuchaguliwa basi chagua. Unakuwa umetutendea haki na ninaamini rafiki yangu Tundu Lissu na wenzake haki ya kuchagua wataitumia vizuri,” amesema Dk.Nchimbi.

Wakati Dk.Nchimbi akieleza hayo kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu jana amefanya kikao na waachama wa Chama hicho katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam na kutoa msimamo wake kuwa bila mabadiliko hakuna uchaguzi na katika hilo hatanii.

Akatoa maelezo kwa wana CHADEMA kuwa wale ambao hawako tayari kufuata msimamo huo milango iko wazi maana hakuna atakayeshikiwa bunduki kulazimishwa ‘No Reform No election’.