Home LOCAL BILIONI 13.46 KULETA MAGEUZI YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI MANGALALI

BILIONI 13.46 KULETA MAGEUZI YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI MANGALALI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na: NIRC, Iringa

Tume ya taifa ya Umwagiliaji (NIRC), imefanya makabidhiano ya mradi wa ujenzi miundombinu ya Umwagiliaji, wenye thamani ya shilingi bilioni 13.46, katika kijiji cha Mangalali, kata ya Ulanda mkoani Iringa.

Mradi huo unalenga kuboresha kilimo kwa wakulima zaidi ya 500, ambao sasa wataweza kuzalisha mazao ya chakula na biashara kwa wingi na kwa tija.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Herry James ameipongeza serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa juhudi za utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji mkoani humo.

Amesema, mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka 2025, utajumuisha ujenzi wa miundombinu muhimu kama mifereji ya zege yenye urefu wa kilomita 5.356, mfereji wa upili wa kilomita 1.812, barabara za mashambani za kilomita 7.170, pamoja na ofisi ya umwagiliaji ya mkoa na nyumba ya makazi ya meneja wa skimu.

“Mageuzi haya ya kilimo katika skimu hii ni kwa ajili ya vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa hili, tuamke tulime kisasa na kupata mazao ya chakula na ya biashara kwa kujipanga kutumia kilimo hiki cha umwagiliaji kubadilisha maisha yenu”, amesema James.

Aidha ametumia hatua hiyo kupongeza juhudi za Tume na kazi nzuri inayoendelea kufanyika.

“Miradi yote ya Umwagiliaji iliyoletwa Iringa inafanya vizuri, naomba mfikishieni salamu Mkurugenzi Mkuu Mndolwa msimamizi wa mkoa Mhandisi Akonaay anafanya kazi nzuri na ndiyo sababu Iringa inafanya vizuri katika sekta ya Umwagiliaji,” amesema.

Kwa upande wake Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Iringa, Peter Akonaay, amesema zaidi ya ekari 125 tayari zipo katika mpango huo wa kilimo cha kisasa, huku mazao kama mahindi, maharage, nyanya, hoho, bamia, na mbogamboga yakiwa yamekusudiwa kuongezewa uzalishaji.

“Mageuzi haya ya kilimo, kupitia kilimo cha Umwagiliaji, yameleta matumaini mapya kwa wananchi wa kata ya Ulanga na mradi huu unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa wakulima wa Mangalali na maeneo jirani”, amesema Akonaay

Naye mkulima Benjamin Gasperi ameishukuru serikali na kusema mradi huo ni tumaini jipya kiuchumi kwao.

Kwa upande wa mkulima mwingine Rebecca Singo, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwakumbuka wakina mama wa Mangalali na kuleta mradi ambao utawakomboa.

Mwisho