Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es salaam, Geofrey Mkinga akizngumza alipokuwa akifungua semina ya siku moja kwa waandishi wa habari iliyoandaliwa na TARURA, Jijini humo.
Mhandisi Mshauri kutoka TARURA Makao Makuu, Pharles Ngeleja akitoa mada, kuelezea manufaa ya kutumia teknolojia ya Barabara na madaraja ya mawe katika semina hiyo.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasilino Serikalini, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Bi. Catherine Sungura, akizungumza alipokuwa akiwakaribisha waandishi katika semina hiyo.
PICHA NA; HUGHES DUGILO
NA; HUGHES DUGILO, DSM
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), umeelezea manufaa ya kutumia teknolojia ya Barabara na madaraja ya mawe ikisisitiza ufanisi wake kiuchumi na kudumu kwa muda mrefu.
Hayo yamebainishwa na Mhandisi Mshauri kutoka TARURA Makao Makuu, Pharles Ngeleja katika semina ya siku moja kwa waandishi wa vyombo vya habari, iliyofanyika leo Machi 27, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Ngeleja amesema kuwa Teknolojia hiyo imeonesha faida mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa ajira, kupunguza gharama za ujenzi, na mahitaji madogo ya matengenezo ya miundombinu hiyo.
‘Teknolojia ya Barabara na madaraja ya mawe imefanikiwa kupunguza ghalama katika kutekeleza miradi hiyo. hadi kufikia Februari mwaka, TARURA imejenga jumla ya madaraja ya mawe 401 nchi nzima, na barabara zenye urefu wa kilomita 28.92 zimejengwa katika mikoa ya Mwanza, Kigoma, Rukwa, na Morogoro, na inatarajiwa kudumu hadi miaka 100’ amesema Mhandisi Ngeleja.
Aidha, ameeleza kuwa miundombinu hiyo ni nafuu kwa mara tano hadi sita ikilinganishwa na madaraja ya kawaida, huku ikipunguza gharama za ujenzi kwa hadi asilimia 80 na kuwa rafiki kwa mazingira, nakwamba mawe hayo upunguza hatari ya wizi wa vifaa vya ujenzi.
Amesema Mikoa kama Kigoma, Singida, Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro, na Arusha imejizatiti katika kutumia madaraja ya mawe, ambapo Kigoma inaongoza katika utekelezaji, akibainisha kuwa TARURA ilikadiria gharama ya miradi ya barabara katika mikoa ya Kigoma, Mwanza, Rukwa, na Morogoro kuwa Bilioni 46, lakini kwa kutumia teknolojia hiyo ilikamilisha miradi hiyo kwa Bilioni 10 tu, jambo linaloonesha utofauti mkubwa wa gharama.
Naye, Meneja wa TARURA Kinondoni Edwin Kabwoto, ameelezea mafanikio ya taasisi hiyo katika kuboresha miundombinu ya barabara wilayani humo, hasa kwa ujenzi wa barabara ya kilomita 3.5 katika eneo la Masaki kwa gharama ya bilioni 5, jambo lililoleta manufaa makubwa kwa wananchi.