Home LOCAL MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA MAWAKILI WA SERIKALI KUZINGATIA UMAHIRI NA UBUNIFU

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA MAWAKILI WA SERIKALI KUZINGATIA UMAHIRI NA UBUNIFU

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amewataka Mawakili wa Serikali kuzingatia umahiri,weledi, ubunifu na ubora pindi wanapotekeleza majukumu yao.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa maelekezo hayo wakati akifunga mafunzo kwa Mawakili wa Serikali tarehe 28 Machi, 2025 Jijini Arusha.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yalilenga kuwakumbusha na kuwajengea uwezo Mawakili hao katika masuala mbalimbali ya kisheria ikiwemo usalama, Uzalendo na kulinda maslahi ya taifa, Uandishi wa Sheria, Ushauri wa Kisheria, utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, Utambuzi wa vihatarishi na namna ya kudhibiti na Wajibu wa Wakili wa Serikali katika Usimamizi wa Mikataba.

*“Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo Mawakili wetu wa Serikali katika maeneo mbalimbali ya kisheria ili Mawakili waweze kutimiza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewataka Mawakili wa Serikali kuyatumia mafunzo hayo kama fursa ya kuboresha utendaji kazi wao, ambapo amewataka wanasheria wote wa Serikali kuzingatia weledi na kuwa na fikra na mitazamo chanya katika kutoa huduma bora kwa wanachi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Johari amewahakikishia Mawakili wa Serikali kuwa mafunzo hayo yatakuwa endelevu, ambapo amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatakuwa yanafanyika kila mwaka kwa lengo la kuwaongezea ujuzi na kuwasaidia Mawakili hao katika kukabiliana changamoto za kisheria wanazokabiliana nazo pindi wanapotekeleza majukumu yao.

*“Napenda kuwafahamisha kuwa mafunzo haya yatakuwa endelevu na tutahakikisha mafunzo haya yanaendelea kuwa bora zaidi.”* Amesema Mhe. Johari.

Sambamba na hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewapongeza Mawakili wote wa Serikali walioshiriki katika mafunzo hayo na kuwataka wakawe mabalozi wazuri kwenye maeneo yao ya kazi, pia alizipongeza Wizara,Taasisi na Idara zilizowaruhusu na kuwawezesha Mawakili hao kushiriki katika mafunzo hayo.

Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yaliyofanyika Jijini Arusha yalianza tarehe 24 hadi 28 Machi, 2025 yamehudhuriwa na takribani Mawakili wa Serikali 380 kutoka katika Wizara, Taasisi, Idara na Halmashauri mbalimbali nchini.