Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari akizungumza katika ufunguzi wa semina ya mawakili wa serikali inayofanyika mkoani Arusha.
Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole akitoa mada katika semina hiyo inayofanyika jijini Arusha.
…………………
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amewakumbusha Mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa haraka, kwa wakati na kwa kuzingatia ubora, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo tarehe 25 Machi, 2025 wakati akizungumza na Mawakili wa Serikali kwenye Mafunzo maalumu kwa Mawakili hao yanayofanyika Jijini Arusha.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewakumbusha Mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa haraka na kwa wakati ili waweze kuiishi kauli mbiu ya weledi na ubora pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi.
*“ili tuifikie na kauli mbiu yetu ya weledi na ubora ni lazima tuwe na tabia ya kufanya kazi kwa haraka na kwa wakati.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ameeleza kuwa mafunzo hayo kwa mawakili wa Serikali yatasaidia kuongeza umahiri kwa Mawakili wa Serikali na kuwawezesha kutoa huduma bora za kisheria zitakazochangia katika kuletea maendeleo kwa Taifa.
*“Ili kuweza kutoa huduma bora za kisheria, kitu cha kwanza kwa Mwanasheria ni kuhakikisha kila jambo analifanya kwa wakati na kuzingatia ubora.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Awali akitoa mada kwa Mawakili wa Serikali Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole ameeleza na kuwakumbusha Mawakili wa Serikali juu ya masuala muhimu ya kuzingatia wakati wanapoishauri Serikali ikiwemo kufahamu muundo na nyaraka mbalimbali za Serikali zitakazo wasaidia kuelewa kwa kina majukumu na shughuli za Serikali.
*“Ili uwe Mwanasheria na mshauri mahiri ni lazima uyafahamu vizuri majukumu ya Serikali.”* Amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria
Katika hatua nyingine Bw. Njole amewakumbusha Mawakili wa Serikali kuzisoma na kuzielewa Sheria zinazosimamia Sekta mbalimbali ili waweze kuwa na wigo mpana wa utoaji wa ushauri kwa Serikali.
*“Kama Mwanasheria unatakiwa ufahamu mfumo wa kisheria wa sekta mbalimbali ili uweze kuwa mbobevu katika masuala ya kuishauri Serikali.”* Amesema Bw. Njole
Naye Jaji Mstaafu Mhe. Sirilius Matupa akichangia mada wakati wa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali amewakumbusha na kuwasisitiza kuhusu weledi katika uandishi na uwasilishaji wa ushauri wa kisheria kwa wadau, ambapo amewasisitiza Mawakili hao kuwa mahiri katika nyanja mbalimbali za kisheria ili waweze kutoa ushauri utakaotatua changamoto zinazoweza kujitokeza.
*“Mawakili wanatakiwa kutoa ushauri kwa kufuata misingi ya kisheria na kuwasilisha ushauri wao kwa weledi ili ushauri wanaoutoa uweze kuwa na tija na kutatua changamoto husika.”* Amesema Jaji Matupa
Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yameandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanafanyika Jijini Arusha kwa siku 5 ambapo yameanza tarehe 24 na yataendelea hadi tarehe 28 Machi, 2025.