Home LOCAL KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA KATIBA NA SHERIA YAPITISHA MPANGO...

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA KATIBA NA SHERIA YAPITISHA MPANGO NA BAJETI YA OFISI YA RAIS-UTUMISHI NA TAASISI ZAKE KWA MWAKA WA FEDHA 2025/26

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepitisha Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zake kwa Mwaka wa fedha 2025/26 baada ya kupitia mafungu yote yaliyo chini ya ofisi hiyo na kujiridhisha.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Florent Kyombo amezungumza hayo tarehe 27 Machi, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Bunge jijini Dodoma alipokuwa akikaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo mara baada ya Wajumbe wa Kamati kujadili na kuridhia taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora.

“Kamati imejadili na kuridhia kupitisha Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zake kwa Mwaka wa fedha 2025/26, niwapongeze kwa maandalizi mazuri yenye uwazi, Kamati inawaasa kuwa na matumizi mazuri ya fedha pale zitakapopitishwa katika vikao vya Bunge la Bajeti ambapo tunaamini mtafikia malengo ya kuwatumikia watanzania kwa maendeleo ya nchi. Mhe. Kyombo amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kwa kuwa na majadiliano mazuri na ofisi anayoiongoza ambayo wanaamini yatawasaidia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa majukumu yao kupitia bajeti hiyo.

Mhe. Mwenyekiti, nitoe shukrani za dhati kwa niaba ya ofisi ninayoiongoza mara zote tumepokea maoni, ushauri na michango mbalimbali kutoka katika Kamati yako inayolenga kuboresha Utumishi wa Umma nchini kwa lengo la kutimiza azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na Utumishi wa Umma uliotukuka.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya ofisi hiyo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amesema Kamati hiyo imekuwa msaada mkubwa wa kuiongoza Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora kwa kuwapatia maarifa mengi kutoka kwa Wajumbe wote wa Kamati hiyo yenye kuboresha utendajikazi.

Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na taasisi zake kwa Mwaka wa fedha 2025/26 umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Maelekezo ya Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26).