Benki Kuu ya Tanzania inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa potofu iliyosambaa katika vyombo mbalimbali vya habari. Taarifa hiyo, iliyochapishwa tarehe 19 Machi 2025, ilidai kuwa Shilingi ya Tanzania ndiyo sarafu inayofanya vibaya zaidi duniani. Taarifa hiyo ilitoa maelezo yasiyo sahihi, ikihusisha mwenendo huo na kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje, ongezeko la deni la taifa, nakisi ya urari wa malipo ya kawaida, pamoja na utekelezaji wa miradi ya miundombinu, ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, ambao bado haujaanza.
Kuhusu mwenendo wa Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani, katika kipindi cha miezi kumi na miwili iliyopita hadi sasa, Shilingi ilishuka kwa asilimia 3.6. Hata hivyo, ni vyema kufahamu kuwa, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2024, Shilingi iliongezeka thamani kwa asilimia 9.51, na kuwa sarafu iliyofanya vizuri zaidi duniani kabla ya kubadilika tena kuanzia Januari 2025. Hali hii inatokana na mzunguko wa msimu wa mabadiliko ya fedha za kigeni nchini na sera ya fedha za kigeni ya Benki Kuu, inayoruhusu kubadilika kwa thamani ya sarafu kulingana na nguvu za soko. Chini ya sera hii, thamani ya Shilingi inaendelea kuamuliwa na nguvu ya soko na upatikanaji wa fedha za kigeni sokoni, huku Benki Kuu ikishiriki kwa kiwango kidogo.
Viashiria vya uchumi wa Tanzania vinaonesha ukuaji mzuri, utulivu wa bei, kupungua kwa nakisi ya urari wa malipo ya kawaida, na uimara wa sekta ya fedha inayosaidia utulivu wa Shilingi ya Tanzania kwa muda wa kati na mrefu. Uchumi ulikua kwa asilimia 5.4 mwaka 2024, na kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazokua kwa kasi zaidi barani Afrika. Mfumuko wa bei umeendelea kuwa thabiti na wa chini, ukifikia asilimia 3.1 mnamo Februari 2025, ikilinganishwa na asilimia 4.6 mwaka 2022. Kinyume na madai yaliyotolewa katika makala iliyochapishwa, deni la taifa bado ni himilivu, ambapo uwiano
wa deni kwa Pato la Taifa ulikuwa asilimia 41.1 mwaka 2023/24, chini ya kiwango cha asilimia 50 kinachopendekezwa na IMF. Nakisi ya urari wa malipo ya kawaida ilipungua kwa kiasi kikubwa kutoka asilimia 3.7 mwaka 2023 hadi asilimia 2.7 ya Pato la Taifa mwaka 2024, kutokana na kuimarika kwa mauzo ya nje, hasa katika sekta za kilimo, madini na utalii. Hii inafafanua kwa nini Shilingi iliongezeka thamani kwa kasi kubwa mwishoni mwa Desemba 2024. Zaidi ya hayo, mwenendo huu unalingana na ripoti zilizochapishwa na Benki ya Dunia, Benki inayowezesha Miamala ya Kimataifa (BIS), IMF, na mashirika ya kimataifa ya ukadiriaji wa mikopo.
Benki Kuu inawahakikishia wananchi kuwa itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuhakikisha utulivu wa bei kwa kutekeleza sera za fedha zinazolenga kudumisha uthabiti wa uchumi, ikiwa ni pamoja na utulivu wa Shilingi ya Tanzania.
Emmanuel M. Tutuba
GAVANA