
WAZIRI wa Fedha Dkt Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa upande wa Serikali kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu walioshiriki Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo Ngazi za juu uliolenga kubadilishana Maarifa,Taarifa na Uzoefu kuhusu Sera na mikakati ya maendeleo ya Nchi wameahidi kuendelea kuenzi ushirikiano uliopo baina yao, na kutekeleza makubaliano waliyoyaweka kwasababu yanakwenda sambamba na Dira ya Taifa,mwelekeo wa Serikali na maono ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Dkt Nchemba ameeleza hayo leo hii Jijini Dodoma Februari 28,2025 mara baada ya Kufungua Mkutano huo wa Majadiliano na Mashauriano baina ya Serikali na Sekta binafsi wakiwemo Wabia wa Maendeleo wakijadili kuhusu Sera na Mikakati ya Nchi na mipango kufikia Dira ya Maendeleo 2050.
Na kuongeza kuwa wamekuwa na vikao viwili kimoja kikiwa ni kikao cha ndani na kingine kikiwa ni kikao cha wazi ambapo kwa ujmla wake katika vikao vyote wamefikia makubaliano na kuweka utaratibu wa namna ya kutekeleza yale yote waliyokubaliana.
“Yote kwa yote kwa upande wa Serikali ambapo Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu walioshiriki wa pande zote za Jamhuri ya Mungano wa Tanzania tumewapa uhakika wenzetu wa moja, kuendelea kuenzi ushirikiano ambao tuko nao pili kuendelea kutekeleza yale tuliyokubaliana kwasababu yanaenda sambamba na dira ya Taifa,yanaenda sambamba na mwelekeo wa Serikali, lakini pia yanaenda sambamba na maono ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu na pia yapo ndani ya utaratibu wa Nchi”.
Dkt Nchemba amesema Serikali kupitia chemba ya Biashara,Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na kituo cha Uwekezaji kati ya sekta binafsi na Umma (CPPP) imeendeleza Majadiliano kati ya sekta ya Umma na sekta binafsi ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika maamuzi.
Pia Dkt Nchemba ambaye ni Mwenyekiti wa Mkutano huo amesema Serikali inaandaa mkakati wa Kitaifa wa Uendelezaji wa Uwekezaji 2025/2026 hadi 2034/2035 ambao utakuwa na mpango wa utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini unaoeleza majukumu ya kila mdau na viashiria vya kupima maendeleo.
Aidha amesema katika Mkutano huo wameongelea masuala ya namna ya kuboresha Mazingira ya Sekta binafsi kwa maana ya uwekezaji na mazingira bora ya kufanya biashara pamoja na kuangazia masuala ya Utawala bora na Haki za binadamu na utafutaji wa vyanzo vipya vya kusimamia miradi ya maendeleo.
“Tumeongelea masuala ya namna ambavyo tutashirikishana,tutaboresha mazingira ya sekta binafsi kwa namna zote kwa maana ya uwekezaji na mazingira bora ya kufanya biashara. Vivyo hivyo tumeongelea masuala ya Utawala bora na masuala ya Haki za binadamu na mengine yanayohusiana na utafutaji wa vyanzo vipya vya kuanza kusimamia miradi ya maendeleo”.
Sambamba na hayo amesema yamejadiliwa mambo ya msingi na ya muhimu yanayojitokeza hasa mabadiliko ya Tabia ya nchi na namna ya kutafuta rasilimali fedha katika kipindi ambacho Dunia hasa katika masuala ya kiuchumi yakiwa hayatabiliki.
Ikiwa ni pamoja kujadiliana na kuelezeana utekelezaji wa yale waliyokubaliana katika vikao vilivyopita.
Mkutano huu umehudhuliwa na Wabia mbalimbali wa maendeleo akiwemo Bi.Suzan Ngongi Mwakilishi kutoka Umoja wa Mataifa na ni moja ya mpango kazi wa Mashirikiano ya Serikali ambayo wamesaini na wabia wa maendeleo na kukubaliana kuwa na kikao cha Mashauriano mara mbili kwa mwaka.