![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Dofoto_20250213_080504050-860x573.jpg)
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila amefanya ziara ya kutembelea na kukagua Soko la Temeke stereo pamoja na kituo cha daladala Buza wilaya ya Temeke na kuwataka wafanyabiashara na wananchi kujiepusha na watu wenye nia mbaya ya kuchafua amani ya nchi kwani amani na utulivu iliyoko ni muhimu kwa masilahi mapana ya umma ikiwemo shughuli za uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!Akizungumza leo Feb 12,2025 kwa nyakati tofauti akiwa anakagua miradi na katika mkutano wa hadhara RC Chalamila amesema mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo ni muhimu kuwa makini na kuepuka vikundi vya watu vinavyofikiria kutumia mwanya wa Siasa kuwashawishi kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwani amani ikipotea shughuli zote za kiuchumi na kijamii haziwezi kufanyika.
Aidha RC Chalamila ametumia nafasi hiyo kuwataka wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuwa wazalendo kwa Taifa lao kwa kuhalikisha wanalipa kodi stahiki kwa ajili ya maendeleo kwani kodi ni muhimu katika kujenga na kuimarisha miradi ya maendeleo
Vilevile akiwa katika kituo kipya cha daladala cha buza kilichojengwa na Serikali lakini bado hakijaleta tija kitokana na kuwa hakitumiki ipasanyo RC Chalamila ameagiza watendaji katika wilaya hiyo kuhakikisha gari haziendelei kupaki barabarani badala yake zipaki kituoni Buza huku akisisitiza suala la biashara kufanyika saa 24.
Sambamba hilo RC Chalamila alipata nafasi ya kusikiliza kero za wananchi na wafanyabiashara kwenye soko la Temeke Sterio ambao wamezungumzia tatizo la miundombinu ya soko kuwa mibovu, kukosa vivuli pamoja na watu kufanya biashara barabarani ambapo amemtaka Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa manispaa kuhakikisha kero hizo zinapatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe Sixtus Mapunda na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bwana Jomari Mrisho Satura wameahidi kushughulikia changamoto zote za wafanyabiashara pamoja na kusimamia mpango wa kufanya biashara saa 24 kwa kuweka taa za kutosha ili kuwe na mwanga nyakati za usiku.
Pia katika hatua nyingine mara baada ya Mkuu wa Mkoa kufanya ziara amehitimisha ziara yake kwa kufanya mkutano wa hadhara eneo la Tandika kituo cha polisi ambapo ameendeleza msimamo wa Mkoa huo kufanya biashara saa 24, kudumisha amani na kila mtu kulipa kodi stahiki kulingana na kipato chake.