Home BUSINESS MSAJILI WA HAZINA NA CAG KUSHIRIKIANA KATIKA USIMAMIZI WA MASHIRIKA YA UMMA

MSAJILI WA HAZINA NA CAG KUSHIRIKIANA KATIKA USIMAMIZI WA MASHIRIKA YA UMMA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu, akizungumza na waandishi wa habari leo, katika kikao kazi cha siku mbili kilichoanza  Jumanne, Februari 25, 2025 katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, iliyopo Kibaha, Mkoani Pwani

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Charles Kichere, akizungumza katika mkutano huo uliofanyika leo, Februari 25, 2025 Kibaha, Pwani.

Kibaha, Pwani, Februari 26, 2025. 

Ikiwa ni sehemu ya dhamira na jitihada za kuhakikisha taasisi na mashirika ya umma yanaongeza mchango katika ustawi wa uchumi wa Taifa, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi zimekubaliana kushirikiana katika maeneo nane ya kiusimamizi.

Maeneo waliyokubaliana kushirikiana ni utawala bora, ufanikishaji wa utekelezwaji wa mapendekezo ya ukaguzi, kuboresha mifumo ya usimamizi na uongozi, usimamizi mzuri wa rasilimali za umma, uwajibikaji wa kifedha., kutekeleza kwa vitendo na kuiishi falsafa ya R 4 za Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. 

Pia, katika kikao hicho kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuongozwa na Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu, pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Charles Kichere, pande mbili zilijadili juu ya haja ya taasisi za umma kukumbatia utendaji unaozingatia sheria, matumizi ya TEHAMA, na mafunzo kwa watumishi yote haya yakilenga uimarishaji wa taasisi na mashirika ya umma. 

Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao kazi cha siku mbili kilichoanza  Jumanne, Februari 25, 2025 katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, iliyopo Kibaha, Mkoani Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 26, 2025, mkoani Pwani, Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu, alisema ili serikali ifanikiwe katika mageuzi inayofanya kwenye taasisi za umma, suala la utawala bora halikwepeki.

“Lazima tuboreshe utawala bora na ndio maana tumeona haja ya kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ambayo ndio yenye jukumu kubwa la kuhakikisha kunakuwa na utawala bora katika taasisi za umma,” alisema Bw. Mchechu.

“Kwa pamoja tumekubaliana kuboresha uhusiano wa kiutendaji kati ya taasisi hizi mbili za serikali. Katika hili tumeona haja ya kuwa na muingiliano “interaction” wa mara kwa mara kati ya menejimenti ya Ofisi hizi mbili.

Kwa kufanya hivyo, Bw. Mchechu alisema ufanisi wa taasisi za umma utaongezeka na hivyo kuongeza mchango wao kwenye mfuko mkuu wa Serikali.

“Tayari kuna tija nzuri, lakini shauku yetu ni kuona taasisi hizi za umma zinaongeza ubunifu na ufanisi ili tupate matokeo chanya ya uwekezaji unaofanywa na Serikali” alisema.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, hadi kufikia Juni 30, 2024, Serikali ilikuwa imewekeza kiasi cha Sh 86.3 trilioni katika taasisi 308 ambazo inazisimamia, ikiwemo zile ambazo ina hisa chache. Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 14.2 ikilinganishwa na Sh75.6 trilioni, kiasi kilichowekezwa hadi kufikia mwaka 2023.

Lengo la Serikali ni kuona Taifa na watanzania kwa ujumla wananufaika na uwekezaji huu wa serikali na ndio maana pamoja na kuongeza uwekezaji, kuna hatua kadhaa tunazichukua ikiwemo kuweka mifumo imara ya usimamizi, uendeshaji na uwajibikaji katika taasisi za umma.

Kwa upande wake Bw. Kichere alisema kikao cha Ofisi yake na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilikuwa na tija kwani walijadili mambo muhimu yanayogusa maslahi ya Taifa.

“Tulijadili kuhusu kuboresha uwajibikaji wa kifedha na utekelezaji  wa maazimio mbalimbali yanayolenga kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora,” alisema Bw. Kichere.

Pia katika Mkutano wa Ofisi hizo mbili walikubaliana kushirikiana linapokuja suala la kuhakikisha taasisi za umma zinatekeleza mapendekezo ya ukaguzi  “Audit recommendations”.

“Katika hili Msajili wa Hazina peke yake hawezi, halikadhalika Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali na ndio maana tumeona haja ya kuzungumza lugha moja,” alisema Bw. Kichere.

Pia, katika orodha ya maeneo ya ushirikiano ni juu ya namna bora ya kuhakikisha taasisi za umma zinasimamia vizuri  rasilimali za umma ili zijiendeshe kwa ufanisi na hivyo kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu.

“Tunataka kuona mashirika ya umma yanapunguza utegemezi na badala yake yawe mstari wa mbele katika kutunisha mfuko wa serikali kuu,” alisema Bw. Kichere.

Ili kuongeza ufanisi, Bw. Kichere pia alisema Ofisi yake na ya Msajili wa Hazina walikubaliana kutengeneza mazingira ya taasisi za umma kukumbatia matumizi ya TEHAMA pamoja na mafunzo kwa watumishi.

“Lazima tuwajengee uwezo watumishi wa mashirika ya umma  na pia hatuna budi kukumbatia matumizi ya TEHAMA ikiwa tunataka kuongeza ufanisi,” alisema.

Bw. Kichere aliongeza: “Tuko tayari kuendelea kubadilishana mawazo na uzoefu na Ofisi ya Msajili wa Hazina ili serikali ifikie malengo yake ya  kuboresha mashirika ya umma.”