Home BUSINESS SERIKALI YAPOKEA GAWIO LA SH. BILIONI 4.35 KUTOKA TAAZAMA

SERIKALI YAPOKEA GAWIO LA SH. BILIONI 4.35 KUTOKA TAAZAMA

Na; Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM

Seikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imepokea Gawio la Shilingi Bilioni 4.35 kutoka Shirika linalosimamia Bomba la mafuta kutoka Tanzania kwenda Zambia (TAZAMA).

Tazama imetoa Gawio hilo baada ya kupita miaka mitano, ambapo mara ya mwisho ilitoa Sh. milioni 681.8 mwaka 2019.

Akizungumza katika hafla ya kupokea hundi ya Gawio hilo iliyofanyika leo Agosti 26,2024 Jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Biteko amesema kitendo hicho ni hatua muhimu kwa Tanzania kwani mradi huo una miaka mingi na sasa matunda yanaonekana.

Amesema Rais Samia alipotembelea Zambia moja ya maelekezo yake ilikuwa ni miradi inayounganisha nchi hizo mbili isimamiwe vizuri ili ilete manufaa kwa nchi zote mbili na angefurahi kuona miradi kama Tazama inaleta situ manufaa ya kikodi bali ichangie kunufaisha maisha ya watu.

“Mara ya mwisho kutoa gawio kwa serikali ilikuwa miaka mitano iliyopita, na sasa tumepokea fedha hizi, tunajivunia maana badala ya kuja na sababu na visingizio kadha wa kadha lakini mmekuja na fedha, kuna baadhi ya taasisi wanakuja na maneno mengi ya kijanja… unajua kulikuwa na Covid, tatizo la Dola lakini nyie hamkuwa hivyo, tunatarajia wakati mwingine kutakuwa na habari njema zaidi,” amesema. Dkt. Biteko.

Aidha ameipongeza Bodi na uongozi wa Tazama kwanza kwa jitihada za kufikia hatua hiyo na kubainisha kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati iko kwenye mazungumzo mazuri ya kuongeza uwekezaji kwenye bomba la Tazama.

“Kama mnavyofahamu tunataka kupanua Bomba lililopo kutoka inchi nane hadi kumi na mbili, na litaanza muda si mrefu ili tusafrishe mafuta mengi kwenda Zambia na baadae kutoka Zambia kwenda Kongo (DRC) na majirani zetu,” ameongeza Dkt. Biteko.

Pia amesema Serikali  inakusudia kuanza ujenzi wa Bomba jipya la inchi 24, ambapo tayari wapo kwenye hatua mbalimbali za manunuzi, nakwamba wanataka kuona nishati hiyo inasafirishwa kwa Bomba badala ya malori.

Kwa upande wa Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu amesema Tazama sasa imeamka ikiwa na miaka takriban 58 tangu kuanzishwa kwake nakwamba mafanikio hayo ni moja ya faida za falsafa – 4R, za Rais Samia za Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi mpya.

“Umri huo kama mtumishi wa umma amebakiza miaka miwili kustaafu, anakuwa kidogo mnyonge mnyonge lakini kwa Tazama badala ya kuwa mnyonge ndio imekuja juu, imekuwa tofauti kidogo,” alisema.

Aipongeza TAZAMA kwa hatua hiyo kubwa waliyofikia na kuwahimiza kuendeleza juhudi walizoanzisha ili mwaka ujao wafanye vizuri zaidi.

Akizungumzia tukio hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Kitila Mkumbo amesema Gawio hilo linadhihirisha jinsi ushirikiano wa nchi hizo mbili ulivyo imara.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here