Usione vyaelea, ujue vimeundwa. Ndivyo ninavyoweza kuutumia usemi huu uliokuwa ukitumika kwa miaka mingi hapa nchini kuelezea kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha Mashirika ya Umma ambayo baadhi yake yalikuwa na hali mbaya kiuchumi.
Labda nieleze jambo moja kabla sijaendelea zaidi, nataka ufahamu kuwa Tanzania ina jumla ya Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala wa Serikali 309 ambayo miongoni mwa mashirika hayo, yapo yale yanayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 lakini pia yapo ambayo Serikali inamiliki hisa chache.
Rais. Samia alipoingia madarakani alikuta Mashirika hayo yakiendelea na shughuli zao kama kawaida kwa mujibu wa sheria lakini baadhi yake yakijiendesha kwa hasara na mengine kushindwa kabisa kujiendesha, ndipo alipoamua kuyanusuru kwa kuyashika mkono na kuyawezesha kifedha huku mengine yakiunganishwa ili kuyaongezea nguvu yaweze kujisimamia.
Hapa ngoja nikukumbushe kidogo ili twende sawa, Mnamo mwezi Disemba 15, 2023 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alitangaza kuzifuta taasisi za umma 4 na kuziunganisha taasisi 16 lengo likiwa ni kuimarisha utendaji kazi wa mashirika hayo ili yaweza kuendelea kutoa mchango katika maendeleo ya Taifa.
Uamuzi huo ulifuatia kutokana na hotuba ya Mheshimwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Bungeni April 22 mwaka 2022 alielekeza kufanyika kwa mapitio na uchambuzi wa kina kwa Mashirika ya umma ili yaweze kujiendesha kwa faida.
Mbali na hilo Rais Samia pia aliyaongezea nguvu baadhi ya mashirika kwa kuyapa fedha na kuokoa miradi iliyosimama kwa muda mrefu.
Moja ya Mashirika hayo, ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo baadhi ya miradi yake ilikuwa imesimama kwa muda mrefu na hivyo kulifanya Shirika hilo kushindwa kutimiza ndoto zake. Hapa nitaweka kituo na kukueleza bayana namna ambavyo Rais Samia alivyoibua matumaini yaliyokuwa yamepotea na kukaa katika hali ya sintofahamu huku majengo ya miradi hiyo ikiwa imebaki kwenye sintofahamu.
NHC inatekeleza miradi yake mikubwa miwili iliyokuwa imesimama ya Kawe 711 na Morocco Square yote ya Jijini Dar es Salaam, kimsingi miradi hii imehuishwa na Rais Samia kwa kutoa kibali kwa NHC kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha ili kuiendeleza miradi hiyo.
UTEKELEZAJI WA MRADI WA MOROCCO SQUARE
Hadi kufikia sasa mradi wa Morocco Square upande wa ubunifu (Design), umekamilika kwa asilimia 100, ambapo kazi za ujenzi zilizofanyika hadi sasa umefikia asilimia 99.
Ujenzi wa majengo ya makazi, hoteli na eneo la biashara umeshakamilika , huku wanunuzi wa nyumba na waendesha biashara za hoteli na rejareja wameshakabidhiwa maeneo yao.
Aidha kwa upande wa majengo ya ofisi, mkandarasi anafanya maandalizi ya kufunga sakafu maalum (raised floor finish) ambapo kazi za nje (extenal works), zimekamilika na kukabidhiwa kwa mshitiri.
Katika mahojiano na waandishi wa habari yaliyofanyika mapema mwezi Julai mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kibali cha kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha na kuwawezesha kurejea site na hatimaye miradi inakwenda kwa kasi.
“Mheshimwa Rais ametuwezesha kuwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hii, kama ule wa Morocco Square ni uwekezaji mkubwa na wa mfano kwani hadi sasa umefikia asilimia 99 kukamilika na tayari kuna huduma zimeanza kutolewa” amesema Abdallah.
Naye Msimamizi miliki katika jengo la Morocco Square, Stanley Msofe amesema mradi huo ni wa kipekee kwani una majengo manne tofauti yaliyojengwa kwenye msingi mmoja, na kwamba huduma mbalimbali zimeanza kutolewa zikiwemo maduka makubwa (Mall’s), ambayo tayari watu wameshaanza kufanya Biashara.
“Katika mradi huu ukienda ghorofa ya pili kuna kumbi za sinema ambapo kwa sasa zipo kumbi 4 kwa ajili ya sinema na tayari mwendeshaji amepatikana,
“Pia kuna Hoteli kubwa na yakisasa yenye vyumba vya kulala 81 ambayo tayari imeshaanza kutoa huduma” amesema Msofe.
Kwa upande wake Meneja wa Uhusiano na Habari NHC, Muungano Saguya, amesema ni jambo la furaha kuona mradi huo mkubwa umekamilika, na kwamba unatoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli mbalimbali za kibiashara na uchumi, na kutoa rai kwa wananchi kuwasiliana na Shirika hilo ili kupata fursa ya kushiriki kwenye miradi yao mbalimbali nchini.
“Natoa rai kwa watanzania wote wanaotaka huduma mbalimbali za Shirika ikiwemo kupangisha nyumba au maeneo ya Biashara kuwasiliana nasi kwani tuna mikoa 23 nchi nzima inayotoa taarifa mbalimbali za Shirika na kupata maelezo ya kina kuhusu huduma zetu, au watuandikie kwa sanduku la Posta 2977 , Dar es Salaam, au 2422 Medeli Magharibi – Dodoma”
Hughes Dugilo
Blogger – Journalist,
Green Waves Media
+255759359119
+255624074728
PICHA MBALIMBALI SEHEMU YA HOTELI YA KITALII YA KING JADA NDANI YA MOROCCO SQUARE