katika kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa mpana juu ya mikopo inayotolewa kwenye Taasisi mbalimbali za fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imekuja na Mpango kabambe kwa kueendesha kampeni maalum iitwayo ‘Zinduka, Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo’
Hayo yameelezwa na Afisa Mkuu Mwandamizi, Kurugenzi ya Usimamizi Sekta ya Fedha, Idara ya huduma ndogo ya Fedha, Bw. Deogratius Mnyamani, wakati wa mahojiano na waandishi wa Habari kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Mnyamani amesema kuwa BoT imekuja na kampeni hiyo ili kuhakikisha elimu inafika kwa wananchi na jamii yote kwa ujumla kwani wametambua kuwa kuna watu wengi wanakopa bila kuzingatia vitu muhimu, nakwamba kampeni hiyo inakwenda kutoa uelewa mpana kwa wananchi kabla ya kuchukua mkopo.
“Changamoto iliyopo kwa sasa ni uelewa mdogo kwa watoa mikopo ya fedha pamoja na watumiaji. Ni vema kuzingatia utaratibu kabla ya kukopa fedha katika Taasisi yoyote jambo ambalo litasaidia kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima” amesema Mnyamani.
Ameongeza kuwa wamegundua watu wengi wanapata shida baada ya kukopa kutokana na kutoelimishwa kuhusu vigezo na masharti wakati wanachukua mikopo, hivyo kampeni hiyo inakwenda kutoa fursa ya elimu kwa mkopaji ili apate muda wa kusoma mkataba pamoja na kupata ushauri kabla ya kuchukua mkopo.
Aidha, amewashauri wakopaji kuhakikisha wanapata nakala ya mkataba wa mkopo kwani unaweza kumsaidia pale inapotokea changamoto ya kutaka kudhulumiwa mali zake na mtoa huduma.
Pia mnyamani amezungumzia changamoto iliyopo ya watoa huduma ya mikopo kwa njia ya mtandao, na kufafanua kuwa BoT kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA na Jeshi la Polisi, wanaendelea kuwatafuta watoa huduma hao ambao wamevunja sheria ya uhuru wa mtu binafsi pamoja na kumtangaza vibaya mtandaoni.