Home BUSINESS BENKI KUU YA TANZANIA (BoT) INA WAJIBU WA KUIKOPESHA SERIKALI

BENKI KUU YA TANZANIA (BoT) INA WAJIBU WA KUIKOPESHA SERIKALI

DAR ES SALAAM 

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekutana na waaandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kutoa elimu kuhusiana na kazi yake ya kuhudumia Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki, Bw. Agathon Kipandula, amesema Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 inatoa nafasi ya kutoa mkopo wa muda mfupi kwa Serikali.

“Mkopo huo, kwa mujibu wa Sheria hiyo unaitwa ‘Advance’ ambao unatolewa ili kurekebisha kushuka na kupanda kwa mapato ya Serikali katika kipindi kifupi na sheria inatamka kuwa ni mkopo wa ndani ya siku 180,” amesema Bw. Kipandula.

Ameongeza kuwa Sheria ya BoT imeweka ukomo wa kuzikopesha serikali zinapokuwa na uhitaji kwamba ni asilimia 18 ya mapato ya mwaka uliopita ya Serikali.

Ukomo huo hukokotolewa tarehe 1 Julai ya kila mwaka.

Vilevile, Mkurugenzi huyo wa BoT, ameeleza kuwa mkopo huo hutolewa kwa ajili ya kuiwezesha Serikali kufanya malipo mbalimbali huku ikisubiri makusanyo yake ya kawaida.

“Huu sio mkopo kama vile mimi nipewe mkopo wa nyumba au wa gari kutoka benki za biashara. Huu sio kwamba Serikali itapewa kiasi cha fedha bali serikali itatumia dirisha hili la Advance ili kuziba nakisi kati ya kukosa fedha jana na kupata kesho,” amesema.

Benki Kuu kama wakala wa huduma za kibenki wa Serikali, hupokea na kutunza amana za Serikali na taasisi za umma, husimamia na kuziendesha akaunti za Serikali, kufanya malipo, kuhamisha pesa kutoka katika akaunti hizo na kutunza mapato ya Serikali pamoja na kuendesha akaunti maalum kwa mujibu wa makubaliano baina ya Benki Kuu na Serikali au taasisi za umma husika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here